Monday, January 24, 2011

JONGWE(MUGABE) ADAIWA KUWA MGONJWA

ZIMEIBUKA taarifa za kutatanisha juu ya hali tete ya afya ya Rais wa Zimbabwe, Bw. Robert Mugabe (87) huku zingine zikieleza kuwa hali yake si nzuri na amelazimika kulazwa hospitalini nchini Malaysia baada ya kufanyiwa

upasuaji kutibu kansa ya kibofu.

Tangu Jumatatu kumekuwepo na taarifa mbalimbali za vyombo vya habari vya kimataifa na mitandao mbalimbali kama vile Sauti ya Amerika, Daily Telegraph, zikinukuu vyanzo mbalimbali vya ndani, serikalini na kwenye chama zikisema kuwa kiongozi huyo wa Zimbabwe ana hali mbaya tangu afanyiwe operesheni hiyo hivi karibuni.


Lakini kwa haraka, maafisa wa Serikali ya Zimbabwe hata wale wa chama chake cha ZANU-PF wamekanusha taarifa hizo, wakisema Rais Mugabe yuko katika mapumziko ya mwaka, ambayo huyafanya Desemba hadi Januari, kila mwaka.


Habari juu ya hali tete ya Rais Mugabe kwa mara hii, zilianza kuripotiwa na Gazeti la Daily Telegraph (Uingereza) la Jumatatu, likisema kuwa kiongozi huyo matata, alikuwa hopsiotali baada ya kufanyiwa operesheni. Ingawa pia haikusemwa kama ilikuwa ni uchunguzi wa afya wa kawaida ama la.


Msemaji wa Rais Mugabe, Bw. George Charamba, alitupilia mbali taarifa hizo, huku mbali ya kusema kuwa kiongozi huyo yuko likizo ya mwaka, amenukuliwa akisema “unaonekana kujua mambo mengi kuhusu rais kuliko mimi mwenyewe ninavyojua…kadri ninavyojua, rais yuko likizo yake ya mwaka na suala hili tuliutaarifu umma, atarudi muda si mrefu,” amenukuliwa Bw. Charamba.


Kwa mujibu wa mtandao wa NewsDay, kwa sasa Makamu wa Rais, John Nkomo ndiye anayekaimu nafasi ya Komredi Mugabe.

Kwa upande wake msemaji wa ZANU-PF, Bw. Rugare Gumbo naye hakutoa kauli tofauti na Charamba, akisema kiuwa hata chama kinajua kuwa rais yuko likizo na si vinginevyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Malysia Bw. Datuk Seri Hishammuddin Hussein, alipoulizwa na waandishi wa habari, juu ya taarifa za Daily Telegraph kuwa Rais Mugabe alikuwa nchini humo, alikataa kukubali wala kukanusha habari hizo.


“Siwezi kukubali wala kukanusha juu ya taarifa hizo,” amenukuliwa waziri huyo katika gazeti la The Malaysian Insider.

Kwa mujibu wa taarifa kadhaa, Rais Mugabe ambaye amekuwa madarakani tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1980, huku akitimiza miaka 87 ifikapo February, 2011, alifanyiwa uchunguzi wa afya yake akiwa likizoni mapema mwezi huu wa Januari.

Kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwepo na uvumi wa mara kwa mara juu ya hali tete ya kiafya ya rais huyo, lakini haijawahi kuthibitika hata mara moja, hali iliyomlazimu kulizungumzia suala wakati fulani na kubeza.


Mwezi Septemba mwaka jana, mbele ya wahariri wa vyombo vya habari nchini humo, akiwa ikulu, kwa mara ya kwanza alizungumzia juu ya uvumi huo wa mara kwa mara juu ya hali tete ya afya yake na kusema “ sijui huwa ninakufa mara ngapi, lakini hakuna hata mmoja amewahi kusema nimefufuka lini.


“Nafikiri hawataki kuzungumzia, maana watalazimika kuzungumzia kufufuka kwangu mara kwa mara na hiyo maana yake ni utakatifu kitu ambacho kitakuwa ni mafanikio kwa mtu ambaye si mtakatifu…Yesu alikufa mara moja na akafufuka mara moja tu, muda wangu utafika, lakini si sasa,” aliwahi kusema Rais Mugabe.

No comments: