Thursday, January 6, 2011

DR. SLAA ATANGAZA MAANDAMANO NCHI NZIMA

Mussa Juma na Moses Mashala, Arusha

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kufanya maandamano nchi nzima, kupinga utendaji wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na ukiukwaji wa taratibu katika chaguzi mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara jana katika viwanja vya NMC mjini Arusha, ambao ulihitimishwa kwa vurugu kubwa na mabomu baada ya wananchi kutaka kwenda kuvamia kituo kikuu cha polisi kwa lengo la kuwatoa wabunge waliokuwa wanashikilia, Dk Slaa alisema sasa wamesitisha mazungumzo ya aina yoyote na serikali ya Kikwete.

"Tumevumilia sana, sasa inatosha...tunataka serikali ya Kikwete isitawalike tena kwani haki hakuna... Tunaomba Jumuiya za Kimataifa zituelewe...Uchaguzi uliopita matokeo yalichakachuliwa tulikaa kimya, lakini sasa basi,"alisema Dk Slaa.

Alisema kitendo cha polisi kujiingiza katika siasa na kukataza mara kwa mara mikutano na maandamano ya Chadema, ni moja ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

"Leo polisi wamemwaga damu, wamekamata hadi wabunge akiwemo kiongozi wa upinzani bungeni (Freeman Mbowe)..Jambo hili lazima likomeshwe,"alisema Dk Slaa.

Dk Slaa, mgombea wa Urais uliopita kwa tiketi ya Chadema, alisema haridhishwi na utendaji wa Rais Kikwete na vyombo vyake kama polisi na wizara mbali mbali.

"Maisha ya watanzania bado ni magumu...serikali inapandisha bei ya umeme...hawataki kutueleza Dowans kwanini walipwe,...tumechoka na lazima wananchi sasa tuamke,"alisema.

Katika mkutano huo, Dk Slaa alilaani kitendo cha kukamatwa wabunge na kupigwa hadi kujeruhiwa wa wananchi, huku akiwasimamisha majeruhi hao jukwaani wakati alipokuwa akihutubia.
Diwani CCM ahamia Chadema
Katika mkutano huo, diwani maarufu wa CCM wa kata ya Sombetini, Alfonce Mawazo alitangaza kujiondoa katika chama chake na kujiunga na Chadema kwa kile alichoeleza kuwa amechoshwa na ukatili wa CCM.

Mawazo ambaye alihamia CCM mapema mwaka juzi akitokea TLP alipokuwa pia diwani wa kata hiyo, alisema amekuwa akiunga mkono sera mbali mbali za Chadema zikiwemo sera binafsi za aliyekuwa mgombea wa Urais wa chama hicho, Dk Willibroad Slaa.

"Naomba niwaeleze wazi kuwa hata katika uchaguzi mkuu mimi ingawa nilikuwa mgombea wa udiwani wa CCM, nilimchagua Dk Slaa,"alisema Mawazo.

Hadi jana jioni vurugu kubwa zilikuwa zinaendelea, huku polisi kadhaa waliokuwa wanawatawanya wananchi, wakipigwa na majengo, kadhaa ya CCM, yaliharibiwa.

Mapambano ya polisi na raia yalilipuka upya yakianzia kwenye mkutano wa NMC pale wananchi walipoonyesha nia ya kwenda polisi kuwakomboa wafuasi wa Chadema waliokamatwa jana mchana wakati wakiandamana.
Polisi wazidiwa, waomba msaada

Katika kile kilichodhihirika kuwa ni polisi kuzidiwa nguvu, kundi la askari liliondoka jana usiku katika chuo cha polisi (CCP) mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kwenda mjini Arusha kuongeza nguvu za kuwadhibiti Chadema.
Askari hao wanafunzi ni wa awamu ya pili, wakilifuatia kundi la wenzao wanaodaiwa kuwa zaidi ya 50 ambao waliondoka CCP Moshi jana saa 11 alfajiri kwenda mkoani Arusha ambako kulizuka vurugu kubwa huku baadhi ya wananchi wakijeruhiwa.MWANANCHI

No comments: