Monday, January 24, 2011

CHIFU KUNAMBI AFARIKI DUNIAMwasisi wa TANU, Chama Cha Mpinduzi na taifa la Tanzania, Chifu Patrick Kunambi amefariki jumamosi alfajiri nyumbani kwake Ubungo Msewe.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Lucas Kunambi, baba yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na alikuwa akihudhuria kliniki ya wagonjwa wa moyo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Marehemu chifu Kunambi alikuwa miongoni mwa waasisi 17, na wanne waliokuwa wamebakia hai, baada ya wengine 13 kufariki dunia.
Marehemu Kunambi alizaliwa Agosti 16,1916 Matombo mkoani Morogoro akiwa mtoto wa mwisho miongoni mwa watoto 11 wa Mzee Kunambi. Baba yake, Chifu, Kunambi alifariki mwaka 1955 akiwa na umri wa miaka 145.
Chifu Kunambi ndiye aliyeongoza mkutano wa Tanu mapema 1955 uliotoka na pendekezo la kumtuma mwalimu Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kukabiliana na Waingereza waliotaka kuchelewesha uhuru wa Tanganyika kwa miaka 25.
Chifu Kunambi ambaye alishika nafasi mbalimbali za uongozi nchini, kitaaluma ni mwalimu ambaye alipata mafunzo Chuo cha ualimu Tabora na Chuo kikuu cha Makerere.
Aidha yeye ndiye alikuwa msajili wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kazi aliyopewa baada ya kurejea nchini akitoka masomoni chuo kikuu cha Duqene, Marekani alikoenda kusomea shahada ya uzamili kati ya mwaka 1962-1964.

RIP CHIEF. PATRICK KUNAMBI(MAZISHI JUMATANO TUNAOMBWA TUHUDHURIE TUMZIKE BABU YETU)

LUKWANGULE

No comments: