Wednesday, January 26, 2011

BODI YA MIKOPO: UVCCM NI WAZUSHI


Boniface Meena

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB), imeurarua Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kutokana na kile ilichokiita ni kutoa taarifa, "za kizushi na za kukurupuka," na kutaka isigeuzwe jimbo la uchaguzi la wanasiasa.Tamko hilo la HESLB chini ya kichwa cha habari, "Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu haihusiki na Migomo ya hivi karibuni katika Vyuo vya Elimu ya Juu," linajibu mapigo ya tamko la UVCCM, lililotaka mapinduzi ndani ya bodi hiyo ikiituhumu kushindwa kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Hata hivyo, ikitoa ufafanuzi wa tuhuma moja hadi nyingine kati ya zilizoelekezwa kwake, bodi ilipiga kombora ikisema, "mmoja wa viongozi UVCCM, amekitolea mfano Chuo Kikuu kishiriki Mkwawa (MUCE) kama mfano, wakati akitoa tamko la kukurupuka dhidi ya bodi bila hata kufanya uchunguzi wa sababu za ndani za migomo ya wanafunzi wa vyuo."

Vijana hao wa CCM katika tamko lao, walisema, “UVCCM umebaini kuna urasimu unaofanywa na watendaji na haiingii akilini, Mkwawa University wagome kwa kutolipwa posho zao na baada ya siku moja walipwe posho zao baada ya kugoma. Jambo hili si utamaduni wa vijana wa Kitanzania, wale wote wanaohusika CCM ichukue hatua,”

Umoja huo ulienda mbali ukisema, hauko tayari kuona vijana wakiendelea kugoma na wale wote wanaotaka kuanzisha utamaduni mpya wa utawala ambao mpaka watu wagome ndipo ufumbuzi upatikane, wapishe.

Lakini, taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, imeonyesha kukerwa na tamko la vijana hao wa chama kilichoshika hatamu ya dola huku ikitua mzigo ikisema , migomo yote iliyotokea katika vyuo vya elimu hivi karibuni haihusiani na bodi hiyo kwa vyovyote.

"HESLB imetaka isigeuzwe jimbo la uchaguzi ambapo kila anayetaka kusikilizwa na wanafunzi wa elimu ya juu, atumie kwa kutoa shutuma ambazo hazijafanywa uchunguzi wa aina yoyote," ilipiga kombora jingine.

Katika tamko hilo, HELSB ilitoa ufafanuzi kwamba wakati mgomo wa MUCE hapo Januari 14, mikopo yao ilikuwa imekwishalipwa kupitia benki tangu Januari 7 mwaka huu, hivyo madai ya malipo hayo yalifanyika baada ya wanafunzi kugoma si kweli na, "ni uzushi mtupu." "Pia wakati wanafunzi wa Chuo kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), kinatangaza kugoma Januari 18 mwaka huu, bodi ya mikopo ilikuwa imekwishafanya malipo ya mikopo hiyo kupitia chuoni tangu Januari 11, hivyo siyo kweli kwamba walilipwa baada ya kugoma,"ilifafanua zaidi sehemu ya tamko hilo.

Kuhusu madai ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), bodi hiyo iliweka bayana kwamba, msimamo wake ni kuwa haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na ambao bodi hiyo haijapokea matokeo yao ya mitihani ya mwaka wa masomo uliopita.

HELSB ambayo imekuwa ikielekezewa makombora ya migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu huku kukiwa na sauti za wadau mbalimbali wakitaka ifumuliwe na kuundwa upya, ilizidi kutoa ngumu ikisema haiwezi kutoa mkopo kwa mwanafunzi mwenye udahili wa zaidi ya chuo kimoja.

"Hivyo, wanafunzi mwenye tatizo hilo wanashauriwa kuwasiliana na vyuo vyao na TCU ili bodi iarifiwe na chuo gani wanaruhusiwa kujiunga nacho," ilisisitiza.

Kuhusu Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM), bodi hiyo ilikwepa tuhuma hizo na kuruka kimanga huku ikisisitiza, si sahihi kulaumiwa bodi hiyo kwa mgomo wa chuo hicho kwani bodi inatekeeza maelekezo ya Serikali ambayo yanalenga kuzuia upandishaji holela wa ada katika vyuo vya elimu ya juu.

Tamko hilo likizungumzia malalamiko ya Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro(MUM), kutaka bodi ilipe ongezeko la ada, HESLB iliweka msimamo thabiti ikisema itaendelea kutumia viwango vya ada vya mwaka wa masomo 2008/2009 kwa mwaka wa masomo 2010/2011, kwa waombaji wapya na wanafunzi wanaoendelea na masomo hadi hapo Serikali itakapoamua vinginevyo.

Kuhusu madai ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), bodi hiyo ilifafanua kwamba itatoa mikopo ya mafunzo ya vitendo kwa programu ambazo vyuo vimezibainisha katika mitaala kuhusiana na mafunzo ya vitendo na si vinginevyo.

"Mikopo ya mafunzo ya vitendo itatolewa tu baada ya bodi kupata taarifa na orodha kutoka vyuoni ikiainisha wanafunzi wanaotakiwa kwenye mafunzo hayo..., muda na mahali wanakokwenda. Hivyo migomo iliyotokea UDOM haina uhusiano na bodi ya mikopo,"ilitua mzigo huo.

Kuhusu matatizo ndani ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), bodi ilizidi kuongeza wingu zito lililogubika chuo hicho, ikisema tatizo la chuo hicho linapaswa kupelekwa TCU.

Tamko hilo lililojaribu kutoa kile kilichoiitwa ufafanuzi wa tuhuma nyingi na za muda mrefu dhidi ya bodi, liliweka bayana kwamba , wanafunzi wanaosoma kwa mfumo wa (Open and Distance Learning) hawana sifa ya kukopeshwa hivyo KIU inatakiwa kupeleka suala lake TCU na siyo bodi.

Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), sehemu ya tamko ilifafanua kwamba, bodi ilifafanua mafunzo kwa vitendo yatatolewa kwa programu ambazo vyuo vimezibainisha katika mitaala kama ndizo zinazohitaji mafunzo kwa vitendo na si vinginevyo. "Pia mikopo katika robo ya pili, kwa ajili ya chakula na malazi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza inatolewa mara baada ya kuwasilisha orodha za wanafunzi waliosajiliwa vyuoni hivyo mikopo haitatolewa pasipokuwa na orodha hiyo."

Hata hivyo, bodi hiyo imelalamika taasisi nyingi za elimu ya juu ambazo wanafunzi wake wanakopeshwa na bodi kwamba zimekuwa zikichelewa kupeleka taarifa muhimu zikiwemo orodha ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliosajiliwa, matokeo ya mitihani na orodha za majina ya wanafunzi wanaokwenda katika mafunzo kwa vitendo.

"Matokeo ya kucheleweshwa kwa taarifa hizo yameibua malalamiko miongoni mwa wanafunzi na hivyo kuelekeza shutuma kwenye bodi bila sababu za msingi,"imeeleza taarifa hiyo.

Hili ni tamko la kwanza kwa mwaka huu kutolewa na HELSB lenye kubeba maudhui mazito kuhusu sababu za migomo katika vyuo vya elimu ya juu, ambayo imekuwa ikiitikisa Serikali na kuifanya itumie nguvu na muda mwingi kuutatua.

Mgomo uliotikisa zaidi ni wa hivi karibuni katika UDOM ambao ukiacha wahadhari kugoma, baadhi ya wanafunzi waligoma na kuandamana wakitaka fedha za kufanyia mafunzo ya vitendo, lakini walielezwa kozi zao hazikuwa na fungu kama ilivyosisitizwa pia na tamko la bodi. Ends


MWANANCHI

No comments: