Saturday, December 11, 2010

ZITTO AVULIWA UONGOZI WA UPINZANI BUNGENI


KAMA ilivyotarajiwa na wengi, mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe amevuliwa wadhifa wake wa unaibu kiongozi wa upinzani bungeni, lakini chama hicho 'kikapigwa jeki' baada ya mfanyabiashara maarufu, Mustafa Sabodo kukipa Sh150 milioni kwa ajili ya kujenga chuo cha maadili ya uongozi.

Matukio hayo mawili pia yaliambatana na kuugua ghafla kwa Zitto na makamu mwenyekiti wa Chadema, Said Amur Arfi ambao wamelazwa Hospitali ya Aga Khan kwa matatizo tofauti.

Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinasema kuwa Zitto, ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa Chadema, alipigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na wabunge wa chama hicho kwenye mkutano wao uliofanyika juzi mjini Bagamoyo.
Hadi jana, hakuna kiongozi yeyote wa Chadema aliyepatikana kuzungumzia hatua hiyo, lakini wabunge waliohudhuria semina mjini Bagamoyo na ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walisema kura hiyo ilipigwa baada ya kujadili kitendo chachake cha kupinga uamuzi wake wa wenzake kumsusia Rais Jakaya Kikwete wakati akitoa hotuba ya kuzindua Bunge la Kumi.

Pia wabunge hao walimtaka Zitto ajieleze kutokana na kitendo chake cha kupinga uamuzi wa pamoja wa kumsusia Rais Kikwete.
Uamuzi wa wabunge hao kumvua uongozi ulikuwa ukitarajiwa na wengi baada ya Zitto kupinga hadharani kitendo cha wenzake cha kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia kuonyesha kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais na kushinikiza kuandikwa kwa katiba mpya na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Uamuzi wa kumsusia Kikwete ulifikiwa na wabunge hao baada ya mjadala mrefu ulioisha kwa kupiga kura. Zitto na wenzake tisa hawakuingia ndani ya ukumbi wa Bunge siku Kikwete alipokuwa akihutubia na baadaye kuitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza kupinga kitendo cha wenzake.

Baada ya Zitto na wenzake kutoingia kwenye ukumbi wa Bunge ili watekeleze uamuzi wa kutoka nje wakati Rais Kikwete akianza kuhutubia, katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema waliosusia uamuzi hao wangechukuliwa hatua na kamati ya wabunge.

Baadaye mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu alitangaza kumwandikia barua Zitto na wabunge wengine tisa ambao hawakuingia kwenye ukumbi wa Bunge siku ya uzinduzi, kuwataka wajieleze kwa kuwa walichofanya ni utovu wa nidhamu.
Wakati taarifa hizo za kuvuliwa uongozi wa Zitto zikibainika, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alilazwa tangu juzi saa 3:00 usiku kwenye Hospitali ya Aga Khan katika kipindi ambacho gazeti moja la kila siku limeripoti kuwepo kwa mpango wa kumuua.

Taarifa zinasema Zitto amelzwa wodi namba 57 iliyo ghorofa ya tatu na tayari amechukuliwa vipimo vyote ingawa madaktari wamesema hawakuona tatizo na kwamba wanasubiri kipimo kikubwa.
Akizungumza na gazeti hili akiwa hospitalini, Zitto aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu na kuugua kwake kwa kuwa ni ugonjwa wa kawaida akiwataka wamuombee apone haraka.
"Watanzania wasiwe na wasiwasi na kuugua kwangu. Hii ni kawaida tu, madaktari wananipa matibabu niombeeni nipone haraka," alisema Zitto.

Alipoulizwa kuhusu mkutano huo, Zitto alisema hawezi kueleza lolote kwa kuwa alipata nafasi ya kuhudhuria siku moja kati ya mbili za mkutano huo.
Wabunge wengine wa Chadema, Lucy Owenya na John Shibuda walifika hospitalini hapo jana kumjulia hali Zitto ambaye alijijengea umaarufu katika Bunge la Tisa kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja.
Zitto amekuwa akionekana kuwa na mwenendo tofauti na mwenyekiti wake Freeman Mbowe. Wakati wa uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka jana, Zitto alitangaza kugombea uenyekiti, uamuzi ambao ungempambanisha na Mbowe, lakini wazee wa chama hicho walimwita na kumshauri aondoe jina lake.

Chaguzi za umoja wa vijana wa chama hicho na baraza la wanawake pia ziliibua makundi yaliyoripotiwa kuwa ni ya wafuasi wa Zitto na Mbowe na chaguzi hizo zilivurugika na kuahirishwa.
Mara baada ya Chadema kuingiza wabunge wengi na hivyo kunyakua haki ya kuunda kambi ya upinzani, Zitto alitangaza kugombea uongozi wa kambi hiyo bungeni, lakini baadaye Mbowe alipewa nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine, makamu mwenyekiti wa Chadema, Said Amur Arfi naye amelazwa wodi namba 29 iliyo ghorofa ya pili kwenye hospitali hiyo na habari ambazo hazijathibitishwa zinasema Arfi anasumbuliwa na matatizo ya kibofu cha mkojo.
Hata hivyo, jitihada za Mwananchi kutaka kuonana na kuzungumza na Arfi hazikufanikiwa jana.
Hata hivyo, Chadema ilipata ahueni baada ya Sabodo kuamua kuipa Sh150 milioni ili ifanikishe azma yake ya kujenga chuo cha maadili ya uongozi kitakachoitwa “Mustafa Sabodo Accademy” na mfanyabiashara huyo, ambaye ni kada wa CCM, akasema ataendelea kukisaidia kwa karibu zaidi chama hicho.

Msaada huo wa Sabodo kwa Chadema ni wa tatu katika kipindi kisichozidi miezi minne baada ya muumini huyo wa siasa za Mwalimu Julius Nyerere kukipatia jumla ya Sh200 milioni kabla na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Akitoa msaada huo jana kwa viongozi wa Chadema na wabunge, Sabodo alisema kuwa huo ni mwanzo na ataendelea kukisadia chama hicho kwa sababu kimeonyesha nia ya kuleta maendeleo nchini.

Alisema malengo ya elimu ni kufanya vitendo na sio kula pesa kama inavyofahamika kwa wengine, hivyo mchango wake wa elimu ameshautoa kwa chama fulani lakini hakuna maendeleo yoyote zaidi ya kupoteza pesa bure na badala yake yanabaki majengo tu badala.
“Hii si mara ya kwanza kutoa mchango kwa kuwa nimeshatoa kwa chama lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika ila kwa hiki chama kimeonyesha kina malengo mazuri," alisema.

Alisema yeye ni Mtanzania na amezaliwa mkoa wa Lindi hivyo anaamua kuchangia chama chochote chenye kuonyesha lengo la kufanya maendeleo nchini na sio ubabaishaji na kwamba chama bora kinajulikana kwa vitendo si maongezi yasiyokuwa na msingi.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema chuo hicho kitakuwa ni cha kwanza nchini chenye lengo la kuwapatia mafunzo viongozi wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali ili wawe na uwezo wa kusaidia jamii.

“Tuna lengo la kuanzisha chuo cha kuwasaidia viongozi wawe bora na sio bora viongozi hivyo leo hii tunatangaza rasmi ujenzi wa chuo hicho na ndani ya miaka mitano utakuwa umeshakamilika," alisema Mbowe.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo Chadema itaendelea kumuenzi Sabodo kutokana na umuhimu wake katika chama hicho na taifa kwa ujumla, kama wanavyoenziwa viongozi wengine.

Alisema Sabodo huwa haogopi kama walivyo wafanyabiashara wengine ambao huwa wanaogopa kuchangia vyama vya upinzani kwa kuhofia usalama wao kutoka serikalini.

“Kipindi cha uchaguzi nilikuwa nawafuata wafanyabiashara ambao ni rafiki zangu, lakini walikuwa wanashindwa kunipa ushirikiano kwa kuniambia wazi kuwa wanaogopa vitisho vya serikali, lakini nilivyomfuata Mzee Sabodo aisaidie Chadema wakati wa uchaguzi, aliniambia niwaite waandishi wa habari ili umma ufahamu mchango wake kwa jamii,” alisema Mbowe.

Naye katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema leo kamati ya chama itakutana na kujadili gharama hizo na kuziweka wazi kwa vyombo vya habari, ikiwa ni changamoto kwa vyama vingine.


MWANANCHI