Thursday, December 23, 2010

UTATA WA URAIA WA ALIYEJILIPUA BOMU MAMLAKA ZIWAJIBIKE
Na Baraka Mfunguo


Kama mtu ambaye anafuatilia habari kila siku, ukisikiliza kiasa cha bwana Albert Alonda Mulanda aliyejilipua kwa bomu wakati akikaguliwa na askari jijini Nairobi nchini Kenya na utata kuhusu uraia wake, ni kama mchezo wa kuigiza.
Mwanzoni vyombo vya habari viliwanukuu maafisa Usalama wa Kenya ambao walidai kwamba mhusika huyo ni Mtanzania kutokana na uthibitisho wa pasi ya kusafiria ya kitanzania aliyokutwa nayo. Kama mtanzania wa kawaida nilijisikia fedheha kubwa kwanza jina la nchi yetu limechafuliwa, mahusiano ya kidiplomasia na wenzetu yatakuwa na utata, pia dhana mbaya itakuwa imejengeka si kwa majirani zetu hata nchi za wengine kwamba watanzania ni magaidi.

Lakini leo tunasikia kwamba bwana Albert Alonda Mulanda si Mtanzania tena ila ni raia wa nchi ya Congo aliyekuwa akiishi katika kambi za wakimbizi nchini Kenya. Kuna maswali mengi ya kujiuliza. Kama bwana Mulanda sio mtanzania amepataje pasi ya kusafiria? Alikuwa ana malengo gani na hilo bomu la kujilipua kwa mkono amelipataje?

Inawezekana akawa ni jambazi akawa ni gaidi lakini ugaidi huo anamfanyia nani ama ametumwa na kikundi gani? Huu ni udhaifu mkubwa katika idara zetu za uhamiaji. Inaonekana Tanzania imekuwa kama kichaka cha kupitishia majangili, wahamiaji haramu, wauza madawa ya kulevya, wawindaji haramu n.k n.k Na wote hawa wanapitia katika ngazi mbalimbali serikalini. Kwa hiyo huu ni udhaifu mkubwa na ninashauri idara ya uhamiaji ianze mara moja kufuatilia uhalali wa pasi ya kusafiria ya bwana Mulanda. Na endapo itathibitika bwana Mulanda ameipata kihalali, basi tujue kwamba kuna udhaifu mahali na idara hiyo inabidi ijisafishe mara moja.

Kwa sasa tunaweza kuwa na ubashiri mwingi. Lakini ubashiri wa blogu hii ni kwamba huyo jamaa ni jambazi/mhalifu ambaye alikuwa kwenye mipango lakini kwa hofu ya kustukiwa akajilipua. Lakini sisi Watanzania inabidi tujiulize huyo jamaa amepata wapi hiyo pasi ya kusafiria?
Na hao waliotuchafua inabidi watuombe radhi

No comments: