Monday, December 27, 2010

RAI YA JENERALI


Barua ndefu ya wazi kwa Jakaya


Mwaka 2005 siku chache baada ya Jakaya Kikwete kushika madaraka ya Rais wa Tanzania kutokana na uchaguzi uliompa ushindi wa Oktoba mwaka huo, nilimwandikia Barua Ndefu ya Wazi kupitia katika gazeti la Rai. Kwa kuwa mazingira ya wakati huo na ya leo yanashabihiana sana, na kwa kuwa bado Barua ile Ndefu ya Wazi ina hoja ambazo zinatukumbusha yaliyopita na kututabiria yajayo, tunairejea barua hiyo ambayo maudhui yake yanabaki yaleyale hata kama imehaririwa hapa na pale kusahihisha makosa ya chapa.Ifuatayo ni sehemu ya sita ya barua hiyo.

Mpendwa Jakaya,

Nimejadili maamuzi yaliyofanywa na mikataba iliyotiwa saini ambayo yanatia shaka juu ya maslahi ya Taifa letu. Nia yangu ni kutufanya sote, kama Watanzania, tutafakari hasara tunayopata kutokana na maamuzi na matendo ya wenzetu wachache waliopewa dhamana ya kutuwakilisha katika maamuzi mbali mbali na ambao wanaelekea kujali shibe yao tu na si shida za watu wetu.

Lakini yako mambo mengine mengi ambayo nayo yanachangia kutudidimiza zaidi katika umasikini bila sababu za msingi ila tu kwamba yamekuwa ni mazoea mabaya ambayo hayapigiwi kelele tena.

Nitachukua mfano mmoja, wa magari wanayotumia wakuu wa Serikali yetu. Tunao mawaziri na naibu mawaziri wapatao 60. Inaelekea kila mmoja wao atapewa, au amekwisha kupewa gari linaloitwa “shangingi”, ambalo nitalipunguza bei na kulipangia shilingi milioni hamsini (50, 000,000/-) ingawaje tunajuwa kwamba bei yake ni zaidi ya hapo. Kwa kuyanunua tu tunatumia shilingi bilioni tatu (3,000,000,000/-)

Idadi ya makatibu wakuu na manaibu wao iko chini ya ile ya mawaziri, tuseme nusu yake. Nao wana magari ya aina hiyo hiyo. Kwa hesabu za kichwani tuseme bei ya jumla ya magari yao ni shilingi bilioni moja na nusu (1,500,000,000/-).

Halafu kila wizara inao utitiri wa wakurugenzi, naibu wakurugenzi na makamishna, wasiopungua 200 wakijumlishwa wote. Iwapo kila mmoja wa hawa atapewa gari ya bei ya nusu ya ile ya waziri au naibu waziri (25,000,000/-), gharama ya jumla itakuwa shilingi bilioni tano (5,000,000,000/-).

Mikoa nayo ina wakuu wake, ambao nao wanatembelea magari kama ya mawaziri. Idadi yao ni 26. Ukiwaongeza maofisa utawala (RAS), wanakuwa 52, na wote hao magari yao ni yale yale. Bei ya jumla ya magari yao ni shlingi bilioni mbili na milioni mia sita (2,600,000,000/-).

Wakuu wa wilaya nao wanatembelea magari hayo hayo, na idadi yao ni zaidi ya 100. Bei yake ni shilingi bilioni tano (5,000,000,000/-). Nao maofisa tawala (DO) ambao watakuwa na magari ya bei nusu ya hiyo, yaani bilioni mbili na nusu (2,500,000,000/-). Kila wilaya ina mkurugenzi mtendaji, ambaye naye analo gari karibu sawa na lile la mkuu wa wilaya, ndiyo kusema jumla ya shilingi bilioni tano (5,000,000 000/-).

Sasa, tuongeze wale maofisa wote ambao kila mkoa unao na kila wilaya inao, na ambao wote wana magari ya aina hiyo hiyo, ukiondoa tofauti ndogo ndogo. Yuko kamanada wa polisi wa mkoa na kamanda wa polisi wa wilaya. Yupo ofisa usalama wa mkoa na ofisa usalama wa wilaya. Wapo wakuu wa idara mbali mbali mkoani na wilayani ambao nao wana magari ya aina hiyo hiyo.

Ndugu Rais, niwie radhi kwani hesabu si kitu changu, na inawezekana kwamba katika kupiga mahesabu haya nimekosea sana kwa kuumua tarakimu na kuzifanya ziwe tofauti na hali halisi. Kwa hili naomba radhi. Lakini sidhani kwamba niko mbali sana na ukweli wenyewe. Aidha najua kuna maeneo mawili au matatu ambayo sikuyagusa, lakini hii ninayoitoa ni mifano tu inayoweza kuwa kielelezo cha tatizo kubwa zaidi kuliko ninavyolieleza.

Sasa, wataalamu wa utawala na menejimenti wanatuambia kwamba gharama kubwa kuhusiana na magari si ile ya ununuzi tu, ingawa na ununuzi una gharama kubwa kufuatana na aina ya gari unaloamua kulinunua. Wanasema kwamba gharama kubwa inatokana na matunzo ya gari linapokuwa katika matumizi, kwa maana ya matengenezo, ununuzi wa vipuri, mafuta ya peteroli na kadhalika.

Niliwahi kupata bahati mbaya ya kufanya kazi chini ya mkuu mmoja ambaye aliambiwa, kwa mujibu wa taratibu za Serikali, kwamba achague moja: Ama apewe posho ya mafuta kila mwezi kwa pesa taslimu, ama gari yake ijazwe mafuta MT Depot kila wiki. Akaamua alipwe pesa taslimu na gari lake lijazwe mafuta. Kwa kuwa alikuwa mkubwa alilotaka lilifanyika, hadi aliposailiwa na Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Serkali (PAC). Wako watu wa aina hiyo serikalini.

Ye yote aliyewahi kuanzisha kijikampuni kidogo tu atakuambia adha ya kuwa na magari ya kampuni, na jinsi anavyoingia gharama kubwa kuyatunza magari ya kampuni yake, hasa pale anapoyakabidhi magari kwa maofisa au madereva wasiokuwa waangalifu katika matumizi na matunzo ya magari hayo. Ndiyo maana makampuni mengi yanaamua kuwakopesha watendaji wake ili wanunue magari yao na wayaangalie na kuyatunza wenyewe.

Najua kwamba Serikali yetu nayo iliamua vivyo hivyo, na ikawakopesha maofisa wake magari ili kuondokana na adha inayotokana na matumizi mabaya ya magari ya Serikali, lakini nini kimetokea? Maofisa wamekopa, wakanunua magari, kisha wakayaegesha nyumbani na wakaendelea kutumia magari ya ofisi. Hili linajulikana wazi wazi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya maofisa hawa.

Hivi sasa magari ya Serikali yanaranda usiku na mchana katika maeneo ambayo hayana uhusiano wo wote na utumishi wa umma, yakitumia mafuta ya walipa kodi. Mengine ni yale yenye nembo zinazoonyesha dhahiri kwamba ni magari ya Serikali, lakini wanayoyatumia hawaoni soni wala hawana woga kutamba nayo katika sehemu za starehe kwa sababu wanajua hakuna lo lote litakalowatokea.

Umejengeka utamaduni kwa ye yote anayekabidhiwa gari la Serikali kuliona kama ni gari lake binafsi na anaweza kulitumia vile anavyopenda. Kama ni kwenda sokoni, kupeleka watoto shule, kwenda pikiniki, kubeba magunia ya mkaa, kutembeza biashara za wakubwa, kwenda likizo nyumbani, alimradi anachotaka bwana au bibi mkubwa.

La kutisha zaidi ni kwamba sasa ni magari hayo hayo ya Serikali na mashirika yake ambayo yanatumika katika matendo ya wizi na ujambazi. Taarifa katika vyombo vya habari zinaendelea kuonyesha kwamba wizi mwingi unaofanyika unayahusisha magari hayo, lakini hatupati taarifa yo yote kuonyesha kwamba wanaowajibika na magari hayo wamechukuliwa hatua zo zote

Hapo awali nimejaribu kuonyesha gharama kubwa za magari haya. Serikali yetu ina magari ya fahari na ya “bei mbaya” kuliko serikali nyingi duniani, jambo ambalo haliendani kabisa na hali ya ufukara wa watu wetu na uchanga wa uchumi wetu. Wakuu wa Serikali yetu wanaendeshwa katika magari ambayo katika nchi zilizoendelea yanaendeshwa na wafanyabiashara wakubwa, wacheza sinema, nyota wa muziki wa pop na wauza unga. Sisi tunapata wapi ukwasi huo?

Wote waliowahi kwenda India wamestaajabu kuona magari wanayotembelea mawaziri wa nchi hiyo, ambayo uchumi wake sasa unaanza kushindana na nchi tajiri duniani. Tukilinganisha kajiuchumi ketu na liuchumi la India, hatuoni haya kwa mambo tunayoyafanya? Kama waziri wa India anaweza kutembelea kijigari “Ambassador” kuna ugumu gani kwa waziri wa “walalahoi” wa Tanzania kutembelea Toyota Mark II?

Tumeingiliwa na ugonjwa wa 4x4 kiasi kwamba ukiangalia msafara wa magari ya wakuu wa Serikali yetu wanapokuwa wanaelekea kwenye shughuli ya pamoja utadhani ni wawindaji wanaelekea mbugani kuwinda. Kila mojawapo ya magari hayo ni sawa sawa na kiwanda kidogo cha kusindika maji ya matunda au kusaga mahindi. Aidha inaelekea kila wizara inajiamulia ni aina gani ya kiwanda imnunulie waziri wake: huyu VX, yule, Lexus, yule Range Rover, na kadhalika. Kwa nini hatuwezi kuwa na aina moja ya gari kwa mawaziri wote na makatibu wakuu wote, na wakuu wa mikoa wote?

Kama vile ilivyo kwa mambo mengi mengine kumekuwapo na minong’ono kuhusu maamuzi yanayosukumwa na utashi wa baadhi ya watu kupata “cho chote” katika ununuzi wa magari haya. Dai moja ni kwamba makampuni ya magari yanatoa vishawishi kwa maofisa wanaofanya maamuzi ili wanunue magari yao ya bei kubwa hata kama hayahitajiki kwa shughuli halisi za ofisi husika. Sina ushahidi kuhusu hili, lakini sidhani kwamba ni jambo lisilowezekana.

Mawaziri na makatibu wakuu wanaishi Dar es Salaam, achilia mbali ile riwaya ya Dodoma kuwa “makao makuu” ya nchi hii. Wote wanaishi mahali ambako kuna barabara za lami, na hawahitaji 4x4. Zinapotokea safari za kwenda vijijini kwa nini zisiwepo 4x4 chache katika MT Depot za kuwahudumia kwa pamoja? Ni lini mawaziri wote waliwahi kuandamana kwenda vijijini kwa pamoja?

Rai yangu ni kwamba wakuu wa serikali ya watu masikini hawana budi kuonyesha kwa matendo hali halisi ya mazingira wanamofanyia kazi, na wasitake kujivisha ufahari na utukufu ambao haufanani na hali za wananchi wanaowaongoza. Wakuu wa Serikali yetu wanalipwa vizuri, angalau wakilinganishwa na wananchi wengine. Wanayo marupurupu mazuri na ya kutosha, tena siku hizi yameboreshwa, ikiwa ni pamoja na pensheni nzuri. Hayo yanatosha.

Hawana sababu ya kujiongezea anasa ambazo athari zake ni kuzidisha gharama za uendeshaji wa serikali na kuwatwisha wananchi mzigo ambao tayari ni mzito mno.

Itaendelea.


RAIA MWEMA

No comments: