Saturday, December 11, 2010

RAI YA JENERALI


BARUA NDEFU YA WAZI KWA JAKAYA - 2

Mpendwa Jakaya,

Nafahamu vyema kwamba unaijua vyema nchi uliyoirithi na dola uliyokabidhiwa. Hata hivyo, halitakuwa jambo baya iwapo nitayakariri baadhi ya masuala makuu ambayo nadhani wewe na sisi raia zako tutakabiliana nayo katika kipindi cha miaka hii mitano ya uongozi wako.

Naamini kwamba hatuna budi kuwa na mjadala wa kudumu kuhusu masuala ya kitaifa, hata kama tayari tunayajua. Binadamu hachelewi kusahau, na hata asiposahau, hakosi kuyazoea mambo yaliyomzunguka na kuyaona kama ya kawaida na yasiyostahili tafakuri ya kina ya kila siku.

Kwanza umerithi nchi yenye “amani na utulivu”. Hii ni kweli, has atukizingatia kwamba tunaishi ndani ya bara lenye misukosuko mingi na ya kila mara. Tumewashuhudia majirani zetu kadhaa wakikumbwa na milipuko isiyoisha na iliyoambatana na vita, ghasia na umwagaji mkubwa wa damu. Hayo, Mwenyezi Mungu ametunusuru, na hatuna budi kushukuru kwa hilo, na kutafuta kila njia ya kuiendeleza hali hii tuliyo nayo, na hata kuiboresha.

Lakini pia umerithi nchi yenye kila aina ya neema inayotokana na maliasili ya kila aina—ardhi nzuri yenye rutuba, maji ya kutosha, misitu, madini na kadhalika. Ni maliasili ambayo nchi nyingi barani Afrika zingefarijika kama zingekuwa nayo, lakini hazina. Ni maliasili maridhawa, ambayo ikifanyiwa kazi inaweza ikawa ni chanzo cha utajiri mkubwa.

Raia wavumilivu

Kubwa zaidi ni kwamba umerithi pia raia wema, walio wengi, watu waungwana na wasikivu kwa viongozi wao, alimradi viongozi wawatendee mema. Na hata viongozi wanaposhindwa kuwatendea mema raia zako bado ni wavumilivu, ni wenye kuvuta subira.

Silika ya Watanzania si kuhamaki mara moja wanapohisi watawala wao hawawatendei mema. Ziko nchi, na unazijua, ambazo raia zake hawachelewi kuingia mitaani kwa maandamano ya rabsha mara tu wanapobaini kwamba watawala wao wanafanya mambo siyo. Hapa kwetu ni nadara hilo kutokea.

Kwako wewe binafsi umekabidhiwa nchi iliyojaa raia wanaokupenda sana, kama ninavyoeleza mwanzoni mwa waraka huu. Unayo karama ya kipekee ambayo wanasiasa wengi huitafuta kwa udi na uvumba, hata kwenda Mlingotini kupiga ramli, lakini wasiipate. Wewe unayo hiyo tunu ya kupendwa na watu wako, na hiyo ni amali kubwa kupindukia kwa kiungozi ye yote wa watu.

Lakini pia umerithi nchi ambayo, pamoja na sifa zote hapo juu, raia zake wamebaki kuwa masikini, na umasikini wao unazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka. Maisha ya Mtanzania wa kawaida yamezidi kuwa duni na ameelemewa na madhila ya kila aina—umasikini, ujinga, maradhi, na sasa rushwa.

Hii si hali nzuri hata kidogo. Hali inayochanganya utajiri wa asili kama tulio nao, na watu wema na wasikivu kwa viongozi wao, pamoja na umasikini unaozidi kujichimbia na kuwafanya wakate tamaa, si hali ambayo inaashiria amani ya kudumu. Hali kama hiyo huzaa mikanganyiko, watu wakachanganyikiwa na wasielewe ni nini hasa kinawafanya waendelee kuwa masikini katika neema iliyowazunguka.

Umasikini katikati ya utajiri

Nadhani ni hayati Bob Marley aliyewahi kuimba, “In the abundance of water, the fool is thirsty.” Katikati ya maji, mpumbavu ana kiu. Hiyo ndiyo hali waliyo nayo Watanzania. Katikati ya neema wao wana njaa, ni wagonjwa, ni wajinga.

Lakini upumbavu unaoimbwa na Bob Marley si wa raia. Huu ni upumbavu unaotokana na watawala wao kushindwa kuwaongoza kwa kuwaonyesha maji yalipo na namna ya kuyateka. Kwa hiyo, ingawaje kiu ni ya wananchi, upumbavu(au uzembe) ni wa watawala.

Hili linadhihirika zaidi tunaposhuhudia watawala wale wale wanaoshindwa kuwaongoza wananchi wao kwenye maji, wao wamekwisha kunywa, siyo tu kukata kiu, bali pia kujimwagia, na kuogelea hadi wengine wanazama, na kuachia maji ya ziada yatiririke kwenye mitaro yasikohitajika, na hata kuoshea mbwa wao, huku wakijua fika kwamba wananchi bado wanakabiliwa na kiu kali. Mbele ya binadamu ni matusi, na mbele ya Mungu ni dhambi ya mauti.

Zipo dalili zisizo shaka kwamba kadri mwananchi wa kawaida anavyozidi kutota katika umasikini ndivyo watawala walafi wanavyozidi kujilimbikizia mali bila woga wala haya. Umeyasema mwenyewe majuzi.

Mtu alikuwa hana cho chote kabla ya kupata nafasi eti ya uongozi, lakini mara anapoipata tu anakuwa ni mtu mwingine kabisa kutokana na ukwasi ambao hawezi kuueleza kama matokeo ya ujira halali alioupata kutokana na utumishi wake.

Kwa maneno mengine, watawala wa aina hii ni wezi na wala rushwa. Nilipokuwa mbunge katika miaka ya mwanzo ya 1990, nilipeleka hoja ya mbunge binafsi ikitaka viongozi walazimike kutoa taarifa za mali zao pindi waingiapo madarakani na pia walazimike huzihuisha taarifa zao mwaka hadi mwaka.

Wapo waliotoa taarifa hizo baada ya hoja kupitishwa na Bunge na kutungiwa sheria, na hata baadhi yao kuzitangaza hadharani, lakini baada ya hapo sijui kama wameendelea kufanya hivyo kila mwaka.

Kilicho dhahiri ni kwamba watu wameendelea kujilimbikizia mali haramu, na inaelekea hakuna wa kuwasaili.

Mafisadi na siasa

Kadri watu kama hawa wanavyozidi kujitajirisha ndivyo matapeli wa kila aina wanavyojiingiza katika kinyang’anyiro cha kutafuta nafasi za “uongozi” ili nao wanufaike. Ndiyo maana tunaona watu wanauza nyumba, mashamba, magari, na kila walicho nacho ili wapate fedha za kununua nafazi ya “kuwatumikia wananchi.”

Kwa kuwa wengi wanahusika na mchezo huu mchafu, na hakuna wa kumsema mwenziwe, ndiyo maana hata rushwa katika uchaguzi imebatizwa jina bandia la “takrima”. Katika upotoshaji wa jumla unaofanyika katika magendo ya siasa, sasa hata lugha yetu ya Kiswahili inapotoshwa, tena inapotoshwa na hao hao wanaodai kuwa “viongozi” wetu.

Iwapo tutaendelea hivi tunavyoenenda tusije tukashangaa tukifika mahali Bunge letu, halmashauri zetu, nafasi zote za uongozi hadi Ikulu, zikashikwa na wanunuzi wa kura. Tukifika hapo tutakuwa tumekwisha, na wala mazungumzo kuhusu “amani na utulivu” hayatakuwa na maana tena.

Nashukuru kwamba umelisemea hili nalo, na umeahidi kwamba utashughulikia suala la matumizi haramu ya fedha katika chaguzi zetu. Wapo wanchi wengi walio tayari kukusaidia katika kuiondosh hatari hii kubwa ambayo huko mbele ya safari ina madhara makubwa. Fedha zinahitajika katika uchaguzi, lakini si kwa matumizi tunayoyashuhudia hivi sasa.

Matendo yote yanayopanua mpasuko uliomo ndani ya jamii, hasa mpasuko baina ya watawala wakwasi wa kupindukia na wananchi masikini hohe hahe, katikati ya kila aina ya utajiri wa asili, hayavumiliki katika jamii yo yote ile. Inakuwa mbaya zaidi inapotokea kwamba watawala walioshiba wanaanza kuwabeza wananchi masikini wanapowahoji wakubwa juu ya matendo hayo.

Waswahili husema, “Njaa mwana malegeza, shibe mwana malevya”. Baadhi ya hao wanaotoa kauli za kebehi zinazotokana na ulevi wa shibe ni wale wale ambao si muda mrefu uliopita walikuwa wakienda miayo ya mlegeo wa njaa. Na iwapo siku moja watapoteza nafasi zao za sasa, si kazi wakarejea miayo yao ya asili.

Hivi, Mheshimiwa Rais, kuna kosa gani kwa wananchi kuhoji ununuzi wa ndege ya kifahari kwa ajili ya matumizi ya Rais wakati usafiri mwafaka unaweza kupatikana kwa gharama nafuu zaidi?

Safari za nje

Kuna mantiki gani katika kuwaambia wananchi kwamba ndege hiyo ikichomoka Dar es Salaam, hiyoo.. hadi Tokyo, hadi New York bila kulazimika kutua? Tokyo na New York imegeuka mikoa ya Tanzania, au tunamchagua Rais ili akatuwakilishe huko?

Ni kweli Rais analazimika kufanya kazi za kimataifa, lakini hizi ni za safu ya pili; safu ya kwanza ni ile ya kazi za nyumbani, ambazo zinahitaji ndege au usafiri mwingine wo wote wa kumfikisha kiongozi wetu Tabora, Songea, Kigoma, Sumbawanga na Bukoba. Mtazamo unaomfanya Rais wetu aonekane kama Waziri wa Mambo ya Nje ni mtazamo potofu unaotokana na upangiliaji tenge wa vipaumbele.

Isitoshe, hata kama kweli upo ulazima wa kununua ndege kama hiyo (nasi kweli hatutaki Rais wetu apande punda kama Bwana Yesu) kuna haja gani ya kuwakebehi wale wanaouliza, wakati sote tuajua jinsi maneno matamu yalivyomtoa nyoka pangoni? Kama si ulevi wa shibe ni nini?

Suala jingine lililoibua kebehi ni lile la “uuzaji” wa nyumba za watumishi wa serikali. Inawezekana nina matatizo, lakini nakiri kwamba kila nilivyojaribu kulitafakari sijapata mantiki yake. Labda mantiki yake ingenielea iwapo wahusika wangetumia lugha inayoeleweka. Jibu lililotolewa, kwamba wote wanaouliza maswali kuhusu nyumba hizo wanalia wivu, si jibu bali ni mzaha mbaya.

Je, ni kweli kwamba uamuzi wa kuuza nyumba hizo ulizingatia mahitaji ya Serikali kuhusu watumishi wake waliopo na wajao? Waliouziwa ni wale waliostahili kuuziwa? Hakuna walioingizwa katika orodha ya kuuziwa wakati hawastahili? Bei ya kuuza ilizingatia bei ya soko, au ilipangwa na hao hao waliouziwa?

Hivi sasa Serikali imekuwa inahaha kukamilisha nyumba kwa ajili ya watumishi wake wapya. Ni nini hasa mantiki ya Serikali kuuza nyumba zake na kisha kuhangaika, kwa njia za zima moto, kujenga nyumba mpya? Je, hao watakaoingia katika hizo nyumba mpya nao watauziwa? Kama jibu ni ndiyo, je, Serikali sasa inaingia katika biashara ya kujenga na kuuza nyumba?

Haya ni maswali yanayoulizwa na watu wengi, na sidhani kwamba jibu lake ni kwamba watu wote wanalia wivu. Binafsi nadhani haya ni maji yaliyokwisha kumwagika, na ambayo hayazoleki. Utaratibu wa kupiga rivasi shughuli nzima unaweza kuwa mgumu sana. Muhimu ni kutambua kwamba jambo lililotendeka si sahihi, na kuweka azma ya kutolirudia huko tuendako.

Itaendelea


RAIA MWEMA

No comments: