Tuesday, December 14, 2010

OUATTARA AONGOZA NCHI AKIWA HOTELINIABIDJAN, Ivory Coast
ALASSANE Outtara, ambaye alitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kuwa mshindi wa mbio za uchaguzi, anaongoza taifa hilo akiwa kwenye chumba cha hoteli chenye uwezo wa kuhifadhi dawati moja kutokana na rais anayemaliza muda wake kung'ang'ania Ikulu.

Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu, rais anayemaliza muda wake, Laurent Gbagbo aliamua kujiapisha na muda mfupi baadaye Ouattara naye akaapishwa na kusababisha kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa uongozi kwenye taifa hilo ambalo limekumbwa na vita ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa na jarida la Time la Marekani, Ouattara hana fursa ya kuingia Ikulu kwa hiyo anafanya vikao vya baraza lake la mawaziri katika mahema yaliyopo nje ya hoteli aliyopo.
Utawala wa Ouattara umechukua ofisi ya meneja wa hoteli ambayo ina mashine ya faksi inayotumika kuwasiliana na na balozi za nchi za nje.

Viwanja vya mchezo wa gofu vilivyo jirani na hoteli hiyo vinaweza kugeuka kuwa kambi ya askari walioasi kutoka kwenye jeshi linalomtii Gbagbo.
Katika eneo hilo la dunia ambalo limekuwa likikabiliwa na migogoro ya mara kwa mara, Ouattara mwenye umri wa miaka 68 sasa alitangazwa kuwa mshindi wa urais na Tume ya Uchaguzi, matokeo yaliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Outtara ameshatambuliwa kuwa rais halali na Marekani, Jumuiya ya Ulaya, Ufaransa, ambaye ni mtawala wa zamani wa taifa hilo, na Umoja wa Afrika.
Anakuwa kiongozi wa pekee duniani aliyeshinda uchaguzi na hajafaidi matunda ya ushindi wake na kuambulia kuyaona majengo ya Ikulu kwa mbali.

Pamoja na kulaaniwa na mataifa mbalimbali duniani, Gbagbo amepuuza kilio chao kwa kile kinachoelezewa kuwa ni uswahiba alio nao na mmoja wa washauri wake wa karibu anayeongoza Baraza la Katiba aliyepindua matokeo ya jimbo aliloongoza Ouattara na kumtangaza Gbagbo na kumpa ushindi rafiki yake.

Akiwa bado kang'ang'ania madarakani, Gbagbo ametangaza hali ya hatari , ikiwa ni pamoja na kufunga mipaka ya nchi na kuzuia vituo vya televisheni kurusha matangazo.

Amekataa wito wa kung'oka madarakani kutoka kwa marafiki zake wa karibu, wanasiasa maarufu na akaenda mbali zaidi kukataa kupokea simu aliyopigiwa na Rais wa Marekani, Barack Obama aliyeambiwa kuwa kiongozi huyo alikuwa amepumzika.
"Tupo katika wakati mgumu kwa kuwa mpaka sasa rais aliyemaliza muda wake anakataa kuondoka Ikulu," alisema Guillaume Soro, aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya Gbagbo na ni mmoja wa mawaziri kadhaa waliojiuzulu kupinga uongozi wa rais huyo.

Tayari Umoja wa Afrika umeisimamisha uanachama Ivory Coast, huku shinikizo la kumtaka Gbagbo kuachia madaraka likiongezeka.
Uamuzi huo wa Umoja wa Afrika umekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na viongozi wa Kiafrika kusema kwamba bwana Gbagbo anapaswa kuachana na juhudi zake za kung'ang'ania madaraka, baada ya duru ya pili ya uchaguzi nchini humo iliyompa ushindi Ouattara.

Mkuu wa Tume ya Afrika inayoshughulika na masuala ya ulinzi na usalama, Ramtane Lamamra aliwaambia waandishi wa habari akiwa jijini Addis Ababa, Ethiopia kwamba uamuzi huo wa kuisimamisha Ivory Coast kushiriki katika shughuli za umoja huo utaendelea hadi Ouattara atakaposhika madaraka.
Uamuzi huo wa jumuia hiyo yenye wanachama 53, unaongeza kutengwa kwa bwana Gbagbo, huku Marekani nayo ikionya kuweka vikwazo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Philip Crowley alisema barua ya rais wa nchi hiyo, Barack Obama aliyomwandikia bwana Gbagbo imeweka wazi kwamba iwapo anafanya uamuzi usio sawa, wataweza kumuwekea vikwazo na watu wake wengine ikiwa ni lazima kufanya hivyo.

MWANANCHI

No comments: