Thursday, December 9, 2010

MIAKA 49 YA UHURUNa Baraka Mfunguo


Ni miaka karibia 50 sasa tangia Tanzania/Tanganyika ipate uhuru wake kutoka kwa Mwingereza aghalabu kuna mafanikio na changamoto kubwa katika nchi yetu. Blogu hii inapenda kuwapongeza waasisi wa Taifa hili pamoja na waliopata kuwa viongozi kwani wao ndio chachu ya kutufanya tuwe kitovu cha amani pamoja wa wananchi wake.

Tulitawaliwa na mkoloni kutokana na udhaifu wa viongozi wetu kushindwa kutambua janja ya mkoloni kwa kupewa mikataba ya uongo na kupelekea mkutano mkubwa wa Berlin wa mwaka 1884- 1885 ambao wakoloni walikutana na kugawana Afrika na sisi ndio chanzo cha kuitwa Tanganyika/Tanzania kuanzia hapo. Tulitawaliwa na mjerumani mpaka mwaka 1919 baada ya mkutano wa amani wa Versaille ambapo nchi yetu iligawiwa kwa Mwingereza kutokana na Ujerumani kushindwa vita na sisi tukawa ndio matunda ya vita hivyo na kutwaliwa na Mwingereza.Harakati za kudai uhuru hazikuanzia wakati wa TAA na TANU bali zilianzia katika maeneo mbalimbali lakini yale ambayo yatakumbukwa ni matukio ya vita vya maji maji 1905-1907 na vile vya chifu Mkwawa vya 1891-1894.

Ni chama cha TANU ambacho kilikuja kuwaunganisha Watanzania pamoja kupitia kiongozi ambaye atabakia kuwa alama ya kukumbukwa Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere. Mwalimu aliacha kazi ya kuajiriwa na mkoloni ya Ualimu akajikita katika siasa na harakati za kudai uhuru akizunguka nchi nzima ambayo ilikuwa na miundombinu duni akiwa na gari ya Land Rover ambayo haikuwa gari ya kifahari. Lakini leo hii ni kinyume chake.

Mwalimu alijenga na kuweka misingi imara ya nchi kwa kuliunganisha taifa tunalojivunia leo hii kama kitovu cha amani nchi isiyokuwa na migawanyiko ya udini, ukabila, rangi, jinsia ama cheo . Kila mtu alimheshimu mwenzake kwa kumuita ndugu. Leo hii ni kinyume chake kutokana na chuki ya viongozi wachache wenye uroho wa madaraka. Na sasa ufa huu unaanza kujionyesha dhahiri.

Naomba niziweke changamoto nizionazo kwa mtazamo wangu kwa kifupi

  • Mmomonyoko wa maadili
  • Kuporomoka kwa kiwango cha elimu
  • Rushwa/Ufisadi
  • Udini/Ukabila
  • Ujinga, Umaskini na maradhi
  • Muungano
  • Taifa tegemezi
  • Vyombo vya dola kutumia kuua demokrasia
  • Uongozi mbovuSiasa za Tanzania ni tofauti kidogo na wenzetu ama majirani zetu. Watanzania ni waoga wa kuuliza maswala ya msingi. Hebu fikiria kiongozi wako anatembelea gari ya shilingi milioni 200 kuliendesha na kulitunza zinahitajika pesa nyingine kama hizo, baada ya miaka kadhaa yanauzwa kwa mnada wa bei ya shilingi milioni 10 bei ya kutupa kabisa wakati pesa hizo zingetosheleza katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

Elimu imeporomoka kwa kiasi kikubwa na hii imechochea kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa vijana. Waalimu wanaofundisha madarasani hawaheshimiwi kutokana na elimu kugeuzwa kuwa ni suala la kibiashara. Leo hii tuna utitiri wa shule ambazo zinajiita ni za kimataifa za bweni ambazo zao lake ni uvutaji wa madawa ya kulevya, ushoga, usagaji na uhuni wa kupindukia. Wazazi wanawapeleka watoto wao shule wakitarajia wanawapatia watoto wao elimu bora kwa kuwapeleka katika shule nzuri kumbe wanawaharibu. Pia kwa kiasi kikubwa Operesheni za JKT zilileta msukumo mkubwa na hamasa ya utaifa kwa vijana na kupunguza mmomonyoko wa maadili pamoja na wito wa watu kukubali kufanya kazi katika mazingira yoyote. Leo hii hakuna kijana anayeweza kukubali kupangiwa kazi ama akafundishe shule za Mtina, Lukumbule, Marumba kule Tunduru mkoa wa Ruvuma ama Mtapika, Mnyambe, Mayanga mkoani Mtwara ataripoti kesho atakuaga anaacha kazi. Leo hii suala kama hili watu watalipangia semina ama workshop kulijadili wakati kila kitu kinaonekana dhahiri. Elimu imekuwa nyenzo ya kuchochea matabaka, chombo cha biashara na anasa . Kwa sasa mtu atajivunia mtoto wake anasoma shule fulani na sio mtoto ana uwezo gani darasani.

Suala la rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, mgawanyo wa rasilimali za nchi,hali ngumu ya maisha, umaskini, maradhi, ujinga, na hili la juzi juzi la ufisadi ni moja kati ya vitu ambavyo wananchi wa kawaida wanakosa majawabu ya msingi. Tanzania ni nchi ambayo imezungukwa na maji . Nikimaanisha mito, maziwa na bahari Lakini leo unaambiwa watu hawana maji safi na salama karibia miaka 50 ya uhuru. Wakinamama wanabebwa na baiskeli ama machela maili nne hadi tano kwenda kujifungua, Wamama wanatembea umbali mrefu kwenda kuteka maji huko wanabakwa na kufanyiwa vitendo viovu hakuna wa kuwasemea kwa sababu akisema atapata fadhaa na mfadhaiko katika maisha yake yote .

Turejee suala la kilimo kwanza, ukitembea katika nchi ya Tanzania ukiangalia jinsi ilivyojaliwa na mwenyezi Mungu unaweza ukalia. Lakini kwa sasa hivi hakuna kiongozi ambaye aliweza kuwa na haiba na mtazamo kama aliokuwa nao Mwalimu enzi zake. Mwalimu alikuwa na mipango endelevu ya kuisaidia nchi. Suala la kilimo kwanza ni kama tuseme halipo ingawa vifaa pamoja na malighafi kwa ajili ya kulifanikisha hilo vimeletwa, nina uhakika kabisa havitamnufaisha mkulima wa kawaida kwa asilimia 100%. Kwa sababu watu hawa hawajaandaliwa, hawajahamasishwa, hawajapewa elimu achilia mbali kuwezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi kama pembejeo na mikopo midogo modogo pamoja na masoko ya mazao yake. Ingawa tunasema mfumo wa sasa ni wa soko huria, serikali inawajibika moja kwa moja kwa wananchi wake hilo halipingiki.

Twende kwenye Viwanda Tanzania sasa hivi hakuna kiwanda zaidi ya vile alivyoviacha Mwalimu ambavyo navyo, vimebinafsishwa na kugeuzwa ama magodown ama viwanda vya maplastiki. Maendeleo ambayo unaweza kuyaona Tanzania ni kuwapo kwa Utitiri wa kampuni za simu na viwanda vya kutengeneza pombe na hata ukikaa kwenye TV kila baada ya dakika utasikia tangazo ama la kampuni ya simu ama bia. Hayo ni maendeleo?

Twende katika mikataba yenye utata ukianzia EPA, Meremeta, Tangold, Richmond, Kiwira, majengo pacha ya BOT, Stendi ya mabasi mikoani Dar na mingineyo mingi. Mikataba hii ilifanywa na watu ambao tuliwaamini na tuliwachagua kwa kura ya ndiyo tukitegemea kwamba watayafanya yale ambayo wengi wetu tulitarajia wayafanye. Lakini ona sasa kizungumkuti kilichopo viongozi wetu wanatumia kigezo cha Usalama wa Taifa. . Bado kuna mikataba mingine ambayo hata ukiiona utapatwa na huzuni. Ukiangalia kwa mfano mikataba ya madini jinsi ilivyofanywa kinyemela. Na anayenufaika sio mwananchi wa kawaida ni hao waliosaini na familia zao huku mwananchi wa kawaida akiathirika na athari za uchafuzi wa mazingira pamoja na unyanyasaji wa hali ya juu( rejea mgodi wa North Mara-Nyamongo)

Twende kwenye suala la uchumi. Mfumuko wa bei kutoka kutoka kwenye tarakimu moja kwenda mbili, shilingi kushuka thamani dhidi ya dola. Sasa hivi tunazungumzia shilingi 1,600 kwa dola moja. Kutokana na hilo vitu vinauzwa kwa bei ya juu, ulanguzi pamoja na uchakachuaji wa mafuta, bidhaa feki. Ushindani usiokuwa sawa kibiashara kutokana na serikali kuyapendelea makampuni ya kigeni kwa kuyatoza kodi ndogo ama kutoyatoza kabisa huku yale ya nyumbani yakibebeshwa zigo la kodi. Serikali yenyewe imekaa kimya na huzinduka pale tatizo linapotokea na maamuzi yanayotolewa ni ya papo kwa papo bila kuangalia athari yaani maamuzi ya zimamoto kwa kiswahili cha mtaani.


Kwa kuhitimisha naweza kusema kwamba Tanzania ni nchi yenye misingi imara iliyojengwa na waasisi wetu. Lakini sasa wapo ambao wanataka kuibomoa (soma UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA. J.K Nyerere).Tunahitaji mabadiliko ya kweli miongoni mwetu na tunahitaji kiongozi mwenye kudiriki kuamua maamuzi magumu. Kwa sasa kazi ni kuangalia jinsi wanavyopigana vikumbo kwa waganga, wanavyofanyiana fitina, wanavyoua albino ili wao wapate uongozi n.k n.k. Wazungu wanasema " Try to think as people around you think because you never know who is your real enemy" Hili ni la kweli kabisa katika siasa za Tanzania hivi sasa.

Hebu angalia kielelezo cha vyombo vya dola kutumika kuua demokrasia TanzaniaMapinduzi ya Zanzibar(Ole wao wale wanaoutukuza utawala wa kisultani na kuwa kigezo cha kutaka Muungano uvunjwe)

< width="480" height="385">

HONGERA TANGANYIKA/TANZANIA......HONGERA WAASISI WETU.

No comments: