Tuesday, December 21, 2010

KWA NINI TANZANIA LIMEKUWA KAMA BUZI LA KUCHUNWA ?  • Ya Dowans ni mfano mmoja tu


Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

KATIKA misemo ya mitaani, buzi ni mwanamume ambaye anajikuta akiamini mapenzi motomoto kutoka kwa mtu ambaye kwake anachotaka ni mafanikio ya kihali na mali. Wakati yeye mwanamme anaamini kweli anapendwa, mwanamke mshukiwa anajua kabisa anachokifanya ambacho ni kuchuma mali na hadhi; huku mapenzi yake ya kweli kabisa yako kwa mtu mwingine.

Mchunaji haoni haya wala aibu na wakati mwingine hutamba kwa wenzake kuwa “anamchuna tu” fulani. Mwanamume ‘anayechunwa’ haamini kuwa ‘anachunwa’, na hakuna kitu anachoweza kuambiwa kuwa ‘anachunwa’ kitakachomfanya azinduke kuwa ‘anachunwa’ – yaani anatumiwa kwa ajili ya mali zake.

Mfano mzuri wa hali hii unadokezwa na wimbo wa zamani wa Vijana Jazz, chini ya Komandoo Hamza Kalala (sikumbuki kama alikuwa na Adam Bakari – Sauti ya Zege). Wimbo ninaouzungumzia ni ule wa “Penzi Halina Umaarufu”. Katika simulizi ndani ya wimbo huo, mume kamnyanyasa mkewe hadi akaamua kuondoka.

Akidhani yeye ni maarufu wa mapenzi, akaamua kumpata mwingine baada ya harusi ya nguvu. Kumbe baada ya muda akagundua kuwa mke huyo mpya alikuwa anamtumia tu kujijenga huko kwao; huku yeye mwanamume akiachwa midabwada (mtupu).

Ndipo kwenye kibwagizo Komandoo Hamza Kalala analalamika na kusema:

Najuta najuta umaarufu umeniponza
mke kaondoka leo namkumbuka
mke kaondoka kumbe penzi halina umaarufu

Huyu niliyeoa, sina la kusema
Mshahara nikipata
Bajeti apange yeye
Anajenga nyumba kwao
Mimi kwangu midabwada

Baada ya taarifa za hukumu ya Dowans kutoka mwanzoni mwa wiki iliyopita, nilipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wenzangu wengine katika kujadiliana maana ya hukumu hiyo na kuangalia kama kuna kitu ambacho kingeweza kufanywa tofauti.

Wengine walinitumia barua pepe na wengine tulizungumza kwa simu. Hata hivyo, mmoja alizungumza kitu ambacho kimenifanya niandikie makala hii ikiwa na maudhui hayo.

Baada ya kuonyeshwa kushtushwa na hukumu hiyo nzito, ndugu yangu huyo ambaye ni kiongozi ndani ya chama kikubwa cha siasa nchini, aliniambia: “Tanzania imekuwa buzi bwana”.

Kwa sekunde kama kumi na tano hivi nilikuwa bado sijaamini nimemsikia sawasawa. Nikamuuliza; “una maana gani mheshimiwa?” akaniambia:

“Kwani huoni? Tangu IPTL hadi Dowans, leo hii, Tanzania imegeuzwa buzi la kuchunwa na kila anayetaka linapokuja suala la nishati.” Tukaendelea kuzungumza na akanipigia hesabu kuwa tangu 1995 Tanzania imetumia karibu Shilingi trilioni 10 kwenye masuala ya nishati na gharama za mafuta kuendeshea majenereta. Akaniambia kuwa katika kipindi hiki wachunaji wamechuna hadi nyama maana ngozi yenyewe ilishaisha zamani!

Lakini nilikataa; nikasema Tanzania haiwezi kuwa kama buzi wakati watu wanajua wanachunwa; nikasema viongozi wetu walio makini na wenye uzalendo hawawezi kamwe kuacha nchi yao ichunwe namna hiyo. Ndipo akaniuliza kwani masuala ya Richmond na Dowans yameletwa na nani?

Kabla sijamjibu akanibambikizia swali la ugomvi – kama hao viongozi wananufaika na uchunaji huo watakuwa wazalendo saa ngapi?

Ndipo na mimi nikaanza kujiuliza maswali niliyopandikizwa na ndugu yangu huyo: Nikafikiria masuala ya Meremeta, EPA, matumizi mabaya ya fedha za umma kwenye wizara, idara na taasisi mbalimbali za umma, mwisho nikajikuta naanza kufikiria inawezekana wachunaji siyo wote ni wawekezaji.

Inawezekana wanaoichuna nchi yetu siyo wote ni wageni na wanaotoka mbali. Yawezekana kati yetu sisi wenyewe wapo ambao wanaona Tanzania ni kama buzi na wanalichuna kama vile wana akili mbovu!

Ndugu zangu, tuna nchi moja tu ambayo kwa haki kabisa tunaweza kuiita ni nyumbani kwetu. Ni mahali hapa pekee katika sayari hii ya dunia na katika makusanyiko haya ya makundi ya nyota kuwa ndipo pekee ni “petu”. Ni hapa ambapo watoto wetu wataturithi na watoto wa watoto wao watawarithi.
Tunapovumilia au kuufumbia macho uchunaji wa nchi yetu kwa sababu ya woga wa kisiasa au kutotaka kuwaudhi wachunaji wakubwa, tunajilaani sisi wenyewe na uzao wetu.

Lakini sisi kama Watanzania hatuna budi kujiuliza kama kinachotokea ni kitu cha kuvumilia au kukificha. Je ni aibu ya nani kuona baadhi ya watu wameigeuza Tanzania kuwa ni “shamba la bibi”? Ni wajibu wa nani kupiga kelele kuwa nchi yetu inachunwa? Je, ni jukumu la walio madarakani peke yao? Je ni jukumu la vyombo vya habari? Je ni jukumu la mwananchi wa kawaida?

Itakuwaje kama mtu wa kawaida anaona ufisadi au ubadhirifu unafanyika na unaligharimu taifa na anajua kuwa akipiga kelele anaweza kupoteza ajira yake? Je, kiongozi ambaye anajaribu kuweka maslahi ya taifa mbele lakini walio juu yake wanamuambia kuwa “mambo ndivyo yalivyo we weka saini tu” afanye nini huyu ili kuzuia nchi yake isiendelee kuchunwa?

Maswali haya yamenifanya nizidi kujiuliza kama sisi sote hatujawa kama Hamza Kalala na kubakia kuimba tu kuwa tumemuacha aliyetupenda kweli tukamleta mwingine, na sasa tumebakia hatuna la kusema.

Fikiria tu kwa mfano; hadi hivi sasa hatujasikia viongozi wetu wakitoa kauli juu ya hili la wabunge kuondoka na vitu vyao na wengine kutoweka na ofisi walizofanyia kazi. Tunasikia kuwa wabunge wanalipwa kiasi cha fedha kwa ajili ya “ofisi zao” lakini hakuna rekodi ya ofisi hizo mahali popote au matumizi. Sasa yawezekana kuwa nchi inachunwa hadi na wabunge wake!?

Katika mazingira hayo, kijana anayeanza ajira serikalini au mtumishi wa ngazi za chini ambaye anasikia na kuona madudu yanayofanywa na walio juu yake au yanayoonekana kuruhusiwa kufanyika na walio juu yake, na yeye hawezi kushawishika kuwa mchunaji? Kwamba, na mtumishi huyu wa kawaida naye kwa namna yake anaamua kushiriki kumchuna huyu buzi aitwaye Tanzania?

Ni nani basi atakayesimama na kupiga kelele za kuwakataliwa wachunaji hawa wanaoimaliza nchi yetu Tanzania?

Hadi hivi sasa inaonekana bado hatujapata jibu la uhakika kwani Tanzania bado inazidi kutafunwa na wenye meno. Kwa kadri tunavyoanza miaka hii mitano ijayo tayari tumeshaanza kusikia kashfa nyingine za mikataba mibovu (Magereza) na ulaji mwingine.

Tusipoangalia siku moja tutajikuta hatuna nchi ya kuwarithisha watoto wetu. Na ilaaniwe siku hiyo na ole wao wale watakaoiona ikija! Lakini ole wao ni wale Watanzania wenzetu ambao kutokana na maamuzi yao au kutokuamua kwao wameifanya nchi yetu kuwa buzi mikononi mwa wachunaji!

Barua-pepe:RAIA MWEMA

No comments: