Tuesday, December 28, 2010

JE VIONGOZI WA IDARA AMBAO NI WACHAGGA WAACHIE NGAZI?
Kumekuwa na chuki za wazi ambazo zisipokemewa kamwe hakutakuwa na Maendeleo Tanzania. Sana sana tutarudi kwenye historia za matatizo ya wenzetu wa Biafra(Nigeria), Rwanda ama Ivory Coast. Siku hizi mtu anakuuliza kabila, akiridhishwa atakuuliza na dini yako. Ila hili la wachagga limepandikizwa siku nyingi na limeshaota mizizi watu wanakuwa sijui tuseme "Insane" au "Paranoid" au ni "inferiority complex" kama ni maendeleo basi tujenge utamaduni wa kujifunza na kujenga kutoka kwa mazuri ya wenzetu wachagga sio kurudishana nyuma. Tunaelekea wapi?Na. M. M. Mwanakijiji


Kuna vumbi la chuki, fitina, wivu, kisasi, na hisia za kibaguzi dhidi ya jamii ya Wachagga nchini. Kuna kila dalili kuwa jamii ya Wachagga nchini siyo tu inaanza kutengwa lakini uwepo wake katika nafasi mbalimbali za uongozi inazua hoja ya ukabila kwa haraka zaidi yawezekana kuliko kabila jingine lolote nchini. Katika Tanzania yetu, wachagga wameanza kunyoshewa kidole siyo kwa siri tena bali kwa wazi kabisa tena na watu ambao wakati mwingine hawapati hata kigugumizi.


Ubaguzi huo msingi wake mkubwa ni idadi ya wachagga katika nafasi mbalimbali za uongozi na hasa kuhusiana na elimu yao. Kuanzia mara tu baada ya uhuru jamii ya wachagga mojawapo ya jamii ambayo watu wake wengi wamesoma sana na kufanikiwa kielimu na kiuchumi imekuwa ikinyoshewa kidole cha kupendelewa.


Mtu yeyote ambaye anaweza akafanya uchambuzi yakinifu hatoshangaa kukuta wataalamu wa kichagga katika nafasi mbalimbali za uongozi au taaluma nchini. Kwenye vyuo vikuu, kwenye idara za serikali na hata kwenye taasisi binafsi kumejaa watu wenye asili ya mkoa wa Kilimanjaro na hususan watu wa jamii ya Kichagga.


Endapo itatangazwa nafasi yoyote ya kitaalamu usishangazwe ukiona kuwa waombaji wengi wana majina ya "Kichagga".


Ni kwa sababu hiyo basi kuna kila dalili kuwa kutokana na wingi wao katika nafasi muhimu na vyeo mbalimbali (hata ndani ya Jeshi la Polisi) Wachagga siyo tu ni wengi lakini wanaonekana kufanikiwa zaidi. Hili ni tishio kwa baadhi ya watu. Ni tishio kwa watu ambao hawako tayari kuangalia jitihada za watu katika kufanikiwa kwao na matokeo yake kushutumu ukabila kila idadi ya Wachagga kwenye kitengo fulani inazidi mmoja.


Ushauri wangu ni kuwa, kwa vile Wachagga wameshasoma sana na kuendelea katika biashara karibu mikoa mingi nchini. Na kwa vile wanaendelea kufanikiwa pia katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini, basi itakuwa vizuri kama watajitolea kuachilia nafasi hizo ili kuwapa nafasi watu wa makabila mengine.


Kwa vile ni wao wanaonekana kulalamikiwa kutokana na mambo ya kifisadi aidha kwa moja kwa moja au kwa kuashiria basi ni vizuri wawape watu wengine nafasi hizo hata kama watu hao hawajasoma sana. Hii yote itakuwa ni katika kudumisha mshikamano, umoja na udugu wa Taifa letu.


Endapo Wachagga wataachilia nafasi mbalimbali kama UCEO, Ukurugenzi, Ukuu wa Idara n.k watasababisha watu wawapende na kuwakubali kuwa ni wazalendo wa kweli. Sitoshangaa kuwa ndugu zetu wa Jamii ya Kichagga wakikaa pembeni, basi ufisadi utakoma serikalini, idara zitaongozwa na watu wazuri, na mara moja na daima Tanzania itaanza kukua katika uongozi.


Kwa kupendekeza nashauri wabunge wote ambao ni Wachagga au wana asili ya mkoa wa Kilimanjaro kuachia ngazi mara moja ili watu wa makabila mengine wapewe nafasi hizo. Siyo wao tu bali pia wabunge ambao wameoa au kuolewa uchagani vile vile wafuate nyazo hizo.


Wakishamaliza hao, wakuu wote wa idara za serikali ambao wana asili ya mkoa wa Kilimanjaro na hasa wa jamii ya kichagga (wamarangu, wamachame, wa Rombo, na wa Kibosho) na wao waamue kuachilia nafasi hizo kwa ndugu zao Wamakua, Wamwera, Wa Ndali, Wadigo n.k Katika hili Wapare hawahusishwi.


Tukishamaliza wakuu hao wa idara za serikali ningependekeza madaktari wote wenye kumiliki hospitali binafsi ambao ni wachagga au wameoa/kuolewa uchagani na wenyewe waamue kuingia ubia na watu wa makabila mengine kama wangengereko, wambuu, na wanjiro ili hayo makabila madogo na wenyewe wapate nafasi ya kujifunza fani hizi muhimu.


Zaidi ya yote, majaji na mahakimu wote ambao wana asili ya Uchaggani na wenyewe waamue kujitoa katika nafasi hizo kwani wingi wao pia unaonekana sana na hivyo kuwa kikwako kwa watu wa makabila mengine kufanikiwa zaidi katika nyanja ya sheria. Kwanza kabisa wale majaji wa Kichagga wa mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu wawe wa kwanza kuweka manyanga chini.


Katika kufanya hivyo jamii ya Watanzania ambao inaona ukabila wa wachagga katika sehemu nyingi itaridhika kwani kwa mara ya kwanza tutakuwa tumeshughulikia chanzo cha matatizo yetu mengi.

JAMII FORUMS

1 comment:

faraji said...

ndugu yangu hilo suala la kusubiri eti wachaga waachie ngazi nafikiri haliwezekani hata kidogo. Ni kweli kuwa wachaga wamejaa kila idara. kitu tunachotakiwa kujiuliza ni kuwa wamefikaje hapo walipo? kumbe badala ya kuwasubiri wachaga washuke chini, tunatakiwa tuwashawishi watu wa jamii zetu kama ulivyowataja (WAMWERA, MAKONDE, MAKUA, ngindo,etc waelimike, wapeleke watoto wao shule,na kuwekeza katika elimu ili kuleta ushindani, na siyo kusubiri aliyeko juu ashuke chini! tubadilike ndugu zangu! chingaz we can! let'z wake up from slumbering!