Kutakuwa na maadhimisho ya siku ya ushirika duniani ambayo kitaifa yanafanyika hapa Mtwara. Hii ni hatua muhimu na ni heshima kubwa ambayo Mkoa wa Mtwara imeupata. Lakini kuna changamoto kubwa ambayo serikali inabidi iitizame kwa umakini kwani inaonekana bado inawanyonya wakulima kwa namna fulani na pia kuwanyima uhuru juu ya mazao yao pamoja na serikali kutowapa wakulima wadogo ushirikiano katika upatikanaji wa pembejeo, mbolea na elimu juu ya kuboresha ubora na upatikanaji kwa uwingi kwa zao la korosho, Pia serikali imeshindwa kumkwamua kiuchumi mkulima kwa kumpa fursa mbalimbali kama vile mikopo na kumshirikisha katika maamuzi ya msingi katika uzalishaji wa zao la korosho. Si katika zao la Korosho pekee hata katika mazao mengine ya biashara na chakula katika mikoa mingine serikali nayo inaonekana kusuasua. Na kinachoonekana ni kama siasa na propaganda katika majukwa. ya kisiasa. Ungana na Rashid Kejo wa Mwananchi katika makala yake ya tarehe 18 Juni mwaka huu. STAKABADHI GHALANI BADO NI WIZI MTUPU!!
Tangazo la taarifa ya ufunguzi wa ununuzi wa zao la korosho lililotolewa na bodi ya Korosho Tanzania kwa msimu wa 2008/2009 lilisomeka kwamba ununuzi huo katika mkoa wa Mtwara utafuata mfumo wa stakabadhi ghalani.
Chini ya mfumo huo, tangazo hilo lilieleza kwamba Korosho zitanunuliwa na Chama cha Msingi cha Ushirika katika Magulio yaliyosajiliwa na kisha kuwalipa wakulima asilimia 70 ya bei ya dira kwa korosho daraja la kwanza ambayo hutangazwa na bei hiyo. Kwa daraja la pili wakulima watalipwa kwa asilimia 100.
"Vyama vya msingi vya ushirika vitakusanya korosho hizo kwa niaba ya wakulima na kuzipeleka kwenye maghala yaliyosajiliwa na serikali ili kutafuta wanunuzi wa korosho. Fedha ya kuwalipa wakulima inatokana na mkopo wa benki kwa wakulima uliodhaminiwa na korosho za wakulima zilizopo maghalani pamoja na garantii wa serikali. Korosho zitauzwa kwa mnada utakaofanyika Mtwara, Ofisi ya Bodi ya Korosho."
"Wakulima watalipwa malipo ya pili ya asilimia 30 baada ya korosho kuuzwa mnadani. Aidha watalipwa malipo ya tatu baada ya msimu kama faida itapatikana kwenye mauzo mnadani...."
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu, Anatoli Tarimo mpango huo wa ununuzi wa Korosho ulitangazwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006, baada ya kusikia kilio cha wakulima cha kudhulumiwa na wanunuzi wakubwa ambao walikuwa wakijipangia bei.
Lakini Tarimo anasema mabadiliko hayo hayakuwa rahisi. Alipata upinzani mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo na hata baadhi ya wakulima ambao walikuwa hawana imani na mpango huo.
" Walikuwa wananizomea nilipokuwa napita kuwaelewesha juu ya mpango huu lakini kwa mara ya kwanza tuliuza na kupata bonasi"
Lakini madai haya ya Mkuu wa Mkoa ni tofauti kwa mkulima huyu wa Nangongo Namwete kijiji cha Malamba Tandahimba ambaye anasema kuwa pamoja na kupata bonasi msimu uliopita wa 2007/2008 mfumo huu hauwasaidii na wala hauwafurahishi na kusisitiza kwamba wakulima wengi wanalazimika kuukubali kwa kuwa ni amri.
Kwa nini? " Tulidhani mnada wenyewe utafanyika mbele ya macho yetu lakini sasa hivi hatujui kinachoendelea. Tulishawahi kuuza korosho mpaka kwa shilingi 800 kwa kilo lakini sasa tumerudi kwenye shilingi 675"
"Tumeanzisha umoja wa wakulima wakubwa wa korosho kwa lengo la kutetea maslahi yetu", anasema Namwete ambaye msimu uliomalizika alivuna tani 10 katika shamba lake lenye ukubwa unaokisiwa kufikia ekari 30 na kuongeza: Msimu ujao nikiona vipi nitakaanga mwenyewe na kuuza rejareja."
Kilio hicho pia kilijitokeza kwa viongozi na wanachama wa chama cha Msingi cha Ushirika cha Matokeo Madaba. Baadhi ya wanachama wanalalamika ya kuwa uwakilishi katika uuzaji wa korosho ni kiini macho kwani baadhi ya vyama vinavyowawakilisha vinasababisha matatizo zaidi.
Lakini Afisa Ushirika wa Wilaya ya Tandahimba, Saidi Munyai anatetea mpango huo akisema kwamba mbali ya mpango huo kudhibiti soko kwa manufaa ya mkulima, umesaidia katika uhifadhi wa korosho kutokana na ukweli kwamba wengi hawakuwa na sehemu nzuri ya kuhifadhi bidhaa hiyo.
"Zamani wanunuzi walikuwa wanawapangia bei wakulima . Lakini leo wanaweza kuja na kusema kilo moja watanunua kwa shilingi 600, kesho wanapunguza mpaka shilingi 500.. Kila siku bei ilikuwa inashuka na mkulima alikuwa hapati faida kama ilivyo sasa" anasema
Lakini Tarimo anawatoa wasiwasi wakulima hao akisema kwamba mnada haufanywi kwa kificho na taratibu zote za manunuzi zinazofanywa zipo kwenye maandishi ambayo wakulima wanaweza kuyapitia na kuhakili ili kujiridhisha.
"Katika hali ya kawaida kwa kweli siyo rahisi kila mkulima kufika eneo la gulio... Wawakilishi wao wapo lakini hapa nina taarifa yote ya mauzo ya korosho yalivyofanyika msimu mzima na taarifa hii siyo ya siri"
Hata hivyo anasema kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi ambao wameanza wizi. Wanachukua mikopo kwa ajili ya kuwalipa wakulima lakini badala yake wananunua pikipiki na kujenga. " Hawa watashindwa kurejesha mikopo hii kwa hiyo ni lazima kusimamiwa kwa karibu. Hiki siyo kitu cha kulala ni kupambana tu kwani wezi ni wengi"
Lakini pamoja na hatua hizo ambazo serikali imechukua, Tarimo anasema mafanikio ya kweli katika udhibiti yatachangiwa kwa kiwango kikubwa na wakulima wenyewe kukataa kunyonywa..
"Maslahi ya wakulima yatatetewa na wakulima wenyewe."
IJUMAA SHOWBIZ!
2 days ago




0 comments:
Post a Comment