Monday, January 5, 2015

CULTURE: NO NIGHT IN ZION
MAMBO 20 MUHIMU YA WANANCHI YALIYOTUPWA NA KATIBA INAYOPENDEKEZWA.
Na  Humphrey Polepole,
Katiba Inayopendekezwa ina mapungufu makubwa na imeyatupilia mbali maoni muhimu ya wananchi kama yalivyotolewa na wananchi wenyewe kama ifuatavyo;-

1. Kupunguzwa kwa madaraka ya Rais
Wananchi walipendekeza madaraka makubwa ya Rais hasa ya uteuzi yapunguzwe na ziundwe Taasisi za kikatiba za kumshauri Rais kabla hajafanya teuzi. Wananchi walipendekeza pia baada ya Rais kumteua kiongozi basi itabidi mteuliwa huyo Bunge limthibitishe. Katiba Inayopendekezwa imeyafuta haya yote na imemuongezea Rais Madaraka.

2. Kutenganisha Mamlaka ya Mihimili ya Dola
Wananchi walipendekeza uhuru zaidi kwa Bunge na Mamlaka zaidi kwa Bunge kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali. Pendekezo hili linaenda sambamba na kutenganisha serikali na Bunge, hali ambayo iko sasa. Rasimu ya Warioba ililipa Bunge Mamlaka zaidi kuisimamia Serikali na hata pale ambapo Bunge lingekataa bajeti au muswada mbaya wa serikali mara kadhaa, Rais asingeliweza kulivunja Bunge. Wananchi walisema sana Mawaziri wasitokane na wabunge, ili wabunge wafanye kazi ya uwakilishi pekee na mawaziri watumie weledi wao kumsaidia Rais kazi za Serikali.

3. Kumwajibisha Mbunge
Rasimu ya Warioba iliwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha Wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati wowote (Recall Powers) kama wakienda kinyume na maslahi ya wananchi katika jimbo husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi wao, iweje hayuko katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze kumwajibisha mpaka miaka mitano?


4. Vyanzo vya Mapato vya kuaminika
Kuwepo kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakavyogharimia mambo ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka 22 hadi 7 lilikuwa pendekezo ambalo hata taasisi za serikali zilipendekeza. Pendekezo la Katiba Inayopendekezwa imerudisha mapato ya Muungano kama Katiba ya Mwaka 1977, na kwa kufanya hivyo tumerudi kwenye mgogoro wa msingi, kuchukua kodi tatu, ushuru wa forodha, ushuru wa bidhaa na mapato kutoka Zanzibar ni kuiua Zanzibar na kuifanya ishindwe kumudu matumizi yake ya ndani kwa mambo yasiyo ya Muungano na vivyo hivyo kwa Tanganyika.


5. Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili
Kwa miaka nenda rudi tumekuwa na kitendawili cha ni muundo gani wa Muungano Jamhuri yetu inao. Kitendawili hiki kimeelezwa na wengi akiwemo Baba wa Taifa Mw. J.K Nyerere. Rasimu ya Warioba iliweka kwa mara ya kwanza Muundo Jamhuri ya Muungano kuwa ni wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili na lenye Serikali 3.


6. Kupunguza ukubwa wa Serikali
Wananchi walionesha kutofurahishwa na ukubwa wa serikali unaopelekea matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi. Walipendekeza uwepo wa serikali ya muungano iliyo imara, yenye ufanisi na ndogo. Rasimu ya Warioba ilisema idadi ya mawaziri isizidi 15, Katiba Inayopendekezwa inasema Mawaziri wasizidi 40


7. Tume ya Uhusiano na Uratibu
Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kunakuwepo uhusiano mzuri, mawasiliano na uratibu wa serikali zote tatu chini ya Mamlaka ya Serikali ya Muungano na kupitia Tume ya Uhusiano na Uratibu. Bunge Maalum lilishindwa kuelewa mantiki ya pendekezo hili na Katiba Inayopendekezwa imelivuruga kabisa, kutoka pendekezo la Warioba la “Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali” hadi “Tume ya Uratibu wa Mambo ya Muungano” katika Katiba Inayopendekezwa.


8. Kupunguza ukubwa wa Bunge
Wananchi walizungumzia pia ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na gharama zinazoambatana nalo, na wakapendeza bunge dogo na lenye ufanisi mkubwa. Warioba alisema idadi ya wabunge isizidi 75, Bunge Maalum likasema Wabunge 390.


9. Ukomo wa vipindi vya ubunge
Wananchi walizungumzia nafasi za ubunge kuhodhiwa na watu fulani kwa miaka nenda rudi na wakapendekeza ifike mahali kuwe na ukomo ili kuleta uwakilishi mpana na mabadiliko. Rasimu ya Warioba iliweka ukomo wa vipindi vya ubunge kuwa vitatu na kuwa na ukomo wa miaka 15 kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Bunge Maalum na Katiba Inayopendekezwa wamefuta pendekezo hili.


10. Kuwepo kwa Tunu za Taifa (Core Values)
Wananchi walipendekeza uwepo wa tunu za Taifa (core values) katika katiba, tunu hizi ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa. Raia wa Tanzania walikuwa na wajibu wa kuheshimu tunu hizi lakini Katiba Inayopendekezwa imezifuta tunu hizi.


11. Maadili na Miiko ya Viongozi
Wananchi walizungumza kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya jamii, watumishi na viongozi wa umma, wengi wakisema Katiba iainishe Maadili na miiko ya viongozi wa umma ambayo kwayo tutawawajibisha. Katiba Inayopendekezwa imesema Maadili na Miiko kwa viongozi (mathalani kutenganisha biashara na uongozi ili kuepusha mgongano wa maslahi), isiwemo kwenye Katiba bali ikawekwe kwenye Sheria.


12. Masharti yasiyoweza kubadilishwa na Bunge
Rasimu ya Warioba iliweka masharti ya kuzuia Bunge kubadili baadhi ya masharti mahususi ya Katiba (entrenched provision) ibara ya 119 isipokuwa kwa ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni (mathalan Malengo Makuu ya Taifa, Haki za Binadamu n.k. Na bahati mbaya tulisahau kuweka na Sura ya 3 juu ya Maadili). Masharti yote ya Ibara hii yamefutwa isipokuwa Muundo wa Muungano na Uwepo wa Jamhuri ya Muungano.


13. Kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi
Wananchi walizungumza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano. Ilisisitizwa juu ya umuhimu wa Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kwamba Mwenyekiti wa Tume na Makamu wake wathibitishwe na Bunge ili kuwapa uhalali wa kitaifa, pendekezo hili limefutwa na Katiba Inayopendekezwa.


14. Usawa wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume
Kuwepo uwiano wa uwalikishi wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume ni lazima kwa mazingira ya sasa. Uwiano kati ya wanawake na wanaume katika vyombo mbalimbali vya dola hasa vile vya kutung sheria limeendelea kuwa tatizo nchini na lililokaa kwa muda mrefu. Wananchi na hasa wanawake na baadhi ya wanaume walipendekeza uwiano ulio sawa katika kufikia fursa hasa ukizingatia wanawake ndio wazalishaji wakubwa. Katiba Inayopendekezwa imefutilia mbali pendekezo hili muhimu.


15. Kuanzishwa kwa Mgombea Huru
Haki ya wananchi kushiriki shughuli za umma imekuwa ikizuiwa siku nyingi na kwamba ushiriki katika shughuli za umma kama kiongozi wa kuchaguliwa inapaswa kuwa haki ya msingi ya mwananchi yeyote yule. Rasimu ilitoa haki ya mgombea huru bila vikwazo, Katiba Inayopendekezwa imeweka masharti magumu ambayo hakuna mtu anayeweza kuyatimiza kirahisi, kitendo hiki sio sawa.


16. Msaada wa Kisheria kwa Wananchi
Wananchi walieleza kutokuridhishwa kwao na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji huo na wakapenda huduma ya msaada wa kisheria liwe suala la kikatiba kwa mwananchi yeyote yule na serikali iwajibike kutoa huduma hiyo. Katiba Inayopendekezwa imesema wananchi hawatakuwa na haki ya kudai huduma hii kokote nchini, hata mahakama hazitaweza kusikiliza mashauri ama Serikali imetoa haki hii au haikutoa haki hii rejea Ibara ya 21.


17. Uhuru wa Mkuu wa Jeshi la Polisi
Rasimu ya Warioba ilipendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi atekeleze kazi zake kwa uhuru, bila woga, upendeleo wala chuki na kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria za nchi. Masharti haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa


18. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Wananchi
Tume ya Warioba ilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania itakayokuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya utumishi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti haya licha ya wapiganaji kupendekeza utaratibu wa kusimamia maslahi yao Kikatiba.

19. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi
Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itakayokuwa na jukumu la kusimamia utumishi wa Jeshi la Polisi. Katika uajiri wa askari wa Jeshi la Polisi, Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itazingatia kanuni na misingi ya utumishi iliyoainishwa katika Katiba hii

20. Misingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi

Rasimu ya Warioba ilipendekeza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano litazingatia (a) viwango vya juu vya kitaaluma na nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wake; (b) ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu; (c) kanuni za uwazi na uwajibikaji; na (d) kukuza mahusiano na jamii. Warioba akaendelea kusema, Jeshi la Polisi, katika kutekeleza majukumu yake, litashirikiana na vyombo vinavyohusika na kupambana na uhalifu vya Nchi Washirika katika kufanya uchunguzi na kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi. Misingi hii yote imefutwa na Katiba Inayopendekezwa

Saturday, January 3, 2015

CHANZO CHA PANYA ROAD: TUSIMTAFUTE MCHAWI.

Heka heka jijini Dar wakati watu wakijilinda usalama wao na mali zao dhidi ya kundi la Panya Road.

Na Baraka Mfunguo,


Panya road walivamia  jiji la Dar  jana  ikidaiwa chanzo chake ni mwanachama mwenzao aliuawa na sungusungu walipokwenda kuiba. Walipitisha michango na mida ya saa kumi jioni walikusanyika magomeni kagera karibu na Friends corner hotel kwa ajili ya mazishi. Kundi kubwa kama la vijana miatano lililosemakana  kuwa  wanasubiri kwenda kwenye mazishi lilikuwa kwenye mkumbo wa kundi Panya Road. Inasemekana walipeana taarifa maeneo yote na viunga vyote vya jiji la Dar  waje kushirikiana  ili  wakimaliza kuzika waanze kulipa kisasi ingawa  haijathibitika kama dhima yao ilikuwa ni kulipiza kisasi ama kuzika ama ni matokeo ya kifo cha mwenzao inayeelezwa aliuawa.


Ilipofika muda wa kwenda kuzika  inaelezwa walifunga barabara na kuanza kuwapora makonda wa daladala na baadhi ya watu huku wakiwa  wakielekea makaburi ya Kagera Mikoroshini, kipindi hicho polisi walipata taarifa na wakapishana nao wao wakidhani wanaenda kuzika katika makaburi ya Mburahati  . Maiti ilizikwa kwa amri  na utaratibu wao huku mashekhe wakishurutishwa na mapanga kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa .


Walipotoka kuzika ikawa wakarudi kupitia njia ya Morogoro road nakuanza uporaji hadi polisi wa kutuliza ghasia  walipofika na kuanza kupiga mabomu, na kufanikiwa kuwakamata wawili.Baada ya kutawanyika, wale waliokuwa wanaoenda mbagala wakawa  wanapora watu ovyo ovyo ,waliokuwa wakielekea Buguruni Tabata na Gongolamboto vivyo hivyo na kundi lililokuwa linadaiwa la Mwananyama ndilo lilirudi tena usiku na kuishia kukabiliana na  polisi wa kutuliza ghasia . 

Vijana  hawa wadogo kiumri  ukiwatazama umri wao unaweza ukakadiria ni  kati ya kuanzia  miaka 14-23 .


Matokeo ya kuasisiwa kwa makundi kama haya ambapo Mtwara lipo kundi maarufu la “Tukale Wapi” ni ni matokeo ya kukosa ajira, rushwa, kukosa elimu na pengo lililopo kati ya walionacho na wasionacho, upendeleo serikalini, hali mbaya ya kiuchumi, kukata tamaa ya maisha, pamoja na wanasiasa kukosa mbinu na ubunifu wa kutatua matatizo yao badala yake wanageuzwa ngazi ya kupandia, ugoigoi wa viongozi na watendaji wa serikali katika kufikiri, NGO's zinazowatumia kama mitaji ya kupata vipato na kuvimbisha matumbo ya wamiliki wake ambao hupita na kujitapa mbele za watu na vyombo vya habari kama wanaharakati. Vile vile  Ufisadi na ukosefu wa maadili kwa viongozi wa nchi pamoja na wale waliopewa dhamana.

Wakati kundi moja likionekana likiwa linaumia, kundi lingine la walionacho linalojumuisha wasomi, wafanyakazi wafanyabiashara, wanasiasa na watu wenye kipato cha kati linaonesha kutojali uhalisia. Jiulize  wewe binafsi ni mara ngapi umekutana na watoto wa mitaani ukiwa barabarani hususan wale wanaojitafutia riziki walau ya kufuta kioo ili wapate ugali  na kuonyesha kutowajali na kufikia hata hatua ya kuwatisha na kuwatolea maneno machafu yasiyoelezeka ama kuandikika. 

Ama kuwahi kusikia maswahibu yao kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na Wizara  pamoja na vyombo vyenye mamlaka husika vipo  pamoja na watendaji wake na havionyeshi kujali na  jibu utakalopewa endapo utataka kujua kwa nini hali ya watoto mitaani inaongezeka kila kukicha  ni, "serikali haijatenga fungu la fedha katika bajeti ya wizara" . Na hata kama serikali ingetenga fungu maalum kwa watoto wa mitaani lingewafikia?  Thubutu! 

Hayo ndio majibu mepesi kwa tukio ambalo sasa linakua na litafikia mahali litawashinda. Sisemi litatushinda kwa sababu sidhani hata mimi ni miongoni mwao. Mimi najichukulia kama raia wa kawaida kabisa kutokana na dhana ya baadhi ya watu wenye madaraka, mamlaka , ajira na kipato kujiona wao wanastahili kuliko wengine. Ni hali halisi ya kibinadamu mmoja mmoja na ubinafsi wa ndani lakini sio hali halisi  ya uhalisia wa maisha ya binadamu kwa ujumla

Wakati wa enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hali haikuwa hivyo kulikuwa na mikakati na mipango dhidi ya watoto wa mitaani na wale watukutu, japokuwa hali haikuwa nzuri kifedha na kiuchumi, lakini iliweza kudhibitiwa . Nakumbuka  pia miaka ya mwanzoni wa tisini nikiwa mwanafunzi wa sekondari ya Tambaza, pale  maeneo Upanga (sikumbuki vizuri mtaa) kama unaenda Zanaki sec ukitokea njia ya DIT(Zamani Dar Tech)  usawa wa  kanisa la Mennonite  kutokea mchepuko Morogoro road mkabala na iliyokuwa shirika la bahati nasibu, kulikuwa hata na mahabusu yao kulikuwa hata  na mjumuisho wa  watoto wa mtaani na watukutu walikuwa marafiki wazuri kutokana na malezi yao na sie tulikuwa tukipita njia  tulikuwa walau tukiwatupia karanga na matunda sasa hivi naambiwa hata magerezani na mahabusu watoto na watu wazima huchanganikana. 

Kimsingi watoto wa mitaani walikuwa hawaonekani na kila mwananchi alijivisha jukumu la kuhakikisha maadili yanakuwepo katika jamii kuanzia ngazi ya chini.

 Sasa imefika wakati huria ambapo watu huweza kuzaana na kutelekeza watoto, wengine kutupa watoto katika mfuko ya plastiki sitaki kusema ya Rambo, watoto kukosa malezi na misingi ya maadili, Elimu kugeuzwa biashara badala ya huduma ya msingi, na hata hizo haki zao zinazoelezwa katika Katiba ibayopendekezwa ni kama porojo tu za wanasiasa. Hao watoto wa mitaani wakiwa wamefikia hatua ya utu uzima yale manyanyaso, uonevu, dhuluma, vitendo vinavyoshusha utu wa mtu ambavyo vinafanywa na hao hao waliomo miongoni mwa watu  wanaojiita wasomi, wanasiasa, wajasiriamali, wanaharakati na watu wa kundi la kati na huku serikali iliwa imefumbia macho matukio hayo, hali  Fulani ya kisaikolojia hujitokeza  inayowafanya wachukie kila kitu na kila mtu.


Wakikutana na watu wakawahamasisha wajiunge na kundi fulani la uhalifu kwa ujira fulani ama kupata ulinzi dhidi ya vitendo vyovyote visivyostahili kufanyika kwao watakataa?Haya yote  kwa mtazamo wangu, inatokana na watu kuchoka mfumo dhulumati, mfumo wa kimafia and "that anger manifest itself into  those actions for them to be heard" hiyo ndiyo fimbo ya mnyonge. 

Mimi binafsi sitashangaa kama haya yakitokea kulikuwa na "Komando Yosso" miaka ya tisini baadae likaja kufa. Ikitokea  Wananchi  wakaamua kuanzisha makundi ya kukabiliana na uhalifu kuna mtu ambaye yuko katika ngazi ya juu serikalini (ukiacha Said Mwema aliyeanzisha polisi jamii ambalo nalo uhalali wake haueleweki mpaka sasa) ataweza kuwapa msukumo na hamasa katika jamii hii ya leo iliyojaa unafiki na uzandiki? 

Tumezoea kuwalaumu Polisi pale matukio mabaya yanayoyowagusa wengi (si mtu mmoja mmoja)yanapotokea Ninaamini  kwa hali hii ya ubadhirifu na ukosefu wa maadili wa viongozi na wale waliohodhi dhamana serikalini kwa njia zao za ghilba na kejeli dhidi ya wananchi, walalahoi na wasionachi,  itafika wakati hata hao panya road wakaonekana mashujaa endapo wakitumika vizuri kuuondoa uozo huu wa rushwa na ufisadi uliojaa na kuifunika nchi gubi gubi na serikali kulala fofofo. 

Pamoja na kwamba  njia walizotumia zinahatarisha usalama wa wananchi na mali zao, ni wakati wa kuchunguza na kubaini chanzo cha matatizo na kukata mzizi na sio tawi kama wengi wanavyotaka iwe. Kukata  tawi kwa mfano ni kuwatafuta kuwakamata na kuwaua, badala yake wawekwe kitako watu waangalie uwezekano wa kuwasaidia na kuwatumia kwa maendeleo ya nchi.